Wafanyakazi
waliokingwa ipasavyo wakifanya kazi za ujenzi katika mradi wa reli ya
kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro katika awamu ya kwanza ya
mradi huo. OSHA huhakikisha kwamba wafanyakazi wanafanya kazi zao katika
mazingira salama
Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye
Ulemavu, Mh. Antony Mavunde, ameupongeza Wakala wa Usalama na Afya
Mahali pa Kazi (OSHA) kwa jitihada unazozichukua katika kuimarisha hali
ya usalama na afya katika sehemu za kazi nchini.
Mh.
Mavunde alizitoa pongezi hizo alipozungumza na wafanyakazi wa OSHA
katika kikao cha pili cha baraza la tatu la watumishi hao kilichofanyika
jijini Arusha mwishoni mwa wiki.
“Niwapongezi
kwa kazi nzuri mnayoifanya katika kuboresha hali ya usalama na afya
katika maeneo ya kazi hapa nchini. Kwakweli kumekuwa na mabadiliko
makubwa sana katika utendaji wenu hasa katika kipindi cha hivi
karibuni,” alisema Mh. Mavunde.
Aliongeza:
“Kipindi cha nyuma mlikuwa mnafanya kazi zenu kama askari polisi jambo
ambalo lilikuwa linawapa hofu kubwa wadau wenu ambao badala ya kuuelewa
wajibu wao kisheria na kuutekeleza, waliishia kuwakwepa na
kuwalalamikia.”
Kiongozi
huyo wa serikali alieleza kwamba kwasasa watumishi wa OSHA wamekuwa
wakijitahidi kufanya kazi kwa weledi mkubwa ikiwemo kuwaelimisha wadau
ili waweze kuutambua wajibu wao kisheria na kuutekeleza bila
kushurutishwa.
Kwa
upande wake Mgeni Rasmi katika kikao hicho ambaye pia ni Katibu Mkuu
(Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Eric
Shitindi, aliwataka watumishi wa OSHA kuendelea kutekeleza majukumu yao
katika namna ambayo itaboresha zaidi huduma kwa wanufaika wake.
“Kipindi
cha nyuma kulikuwa na malalamiko mengi sana kutoka kwa watu
tunaowahudumia lakini kwasasa malalamiko yamepungua sana. Hivyo nawaomba
muendelee kutoa huduma nzuri kwa wateja wenu kwa kuzingia vyema Sheria
na Kanuni mbali mbali zilizopo,” alisema mgeni rasmi.
Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Wakala, Khadija Mwenda, alisema kikao hicho cha baraza
la wafanyakazi kinalenga kufanya tathmini ya utendaji wa taasisi kwa
kipindi kilichopita na kuweka mikakati ya kujiimarisha zaidi kiutendaji
kwa kipindi kijacho.
Wakala
wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni taasisi ya serikali yenye
dhamana ya kusimamia masuala ya Usalama na Afya za wafanyakazi
wanapokuwa katika sehemu zao za kazi. Wakala hufanya kaguzi za kiusalama
na afya katika sehemu zote za kazi hapa nchini. OSHA pia huwashauri
wamiliki ama wasimamizi wa maeneo ya kazi juu ya uwekaji na usimamizi wa
mifumo ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi wanapokuwa kazini.
0 comments:
Post a Comment