Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Morogoro.
Jumla
ya wafanyakazi 252 wa Halmashauri mbalimbali kutoka Mikoa ya Pwani,
Morogoro, Kilimanjaro na Arusha wamepata mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa
wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao
kama PlanRep yanaoendelea mkoani Morogoro.
Takwimu
hizo zimetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Msaidizi wa Miundombinu ya
TEHAMA – TAMISEMI, Baltazar Kibola wakati akizungumza na mwandishi wa
habari hii kuhusu mafunzo hayo.
Kibola
amesema kuwa mfumo huo sio mpya ila umeboreshwa kwa kuongezewa vitu vya
muhimu vitakavyomaliza mapungufu yaliyokuwa yakitokea katika mfumo wa
zamani hali iliyosababisha kudhoofika kwa utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Mfumo
huu ulikuwa ni mfumo unaojitegemea haukuweza kusambaza taarifa katika
ngazi mbali mbali za Serikali wala kushirikisha watoa huduma kutoa
mapendekezo yao yatakayoongeza uboreshaji wa mipango na Bajeti za
Serikali hivyo kwa kuwa tumeuboresha ni wazi kuwa watumiaji wa mfumo huu
wanatakiwa kupewa mafunzo,” alisema Kibola.
Kibola
ameongeza kuwa katika mradi huo Ofisi ya Rais, TAMISEMI imejikita
katika kuratibu utengenezaji wa mfumo huo, kuandaa mafunzo katika mikoa
mbalimbali ambayo imepangwa kwa ajili ya kufanyia mafunzo na kutafuta
wataalam wa TEHAMA pamoja na wawezeshaji pia kuhakikisha vifaa vya
TEHAMA vinakuwepo.
Nae
mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Christopher Masaaka amesema kuwa
asilimia kubwa ya watumiaji wa mfumo wameyapokea vizuri mafunzo hayo
kwani mfumo huo unakwenda kurahisisha uandaaji wa mipango na bajeti
zinazoandaliwa kila mwaka ambazo zilikuwa zikitumia muda mwingi na
gharama kubwa katika maandalizi yake.
“Washiriki
wamefanya vizuri katika mafunzo, wameweza kupanga mipango kutoka ngazi
ya Vituo, Idara, Halmashauri, Mikoa hadi Wizara kama majaribio pia
wameweza kuandaa na kufanya uchambuzi wa mipango na bajeti kupitia mfumo
huo,” alisema Masaaka.
Aidha,
Masaaka ametoa rai kwa Serikali kuongeza nguvu na jitihada zaidi kwa
kuweka miundo mbinu ya TEHAMA na kutoa mafunzo kwa ajili ya kuwajengea
uwezo watumiaji katika ngazi zote ili matumizi ya mfumo huo yakaweze
kuleta matunda mazuri.
Mafunzo
hayo yameandaliwa kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Shirika la
Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) chini ya Mradi wa Uimarishaji
wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).
0 comments:
Post a Comment