Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Morogoro.
Wafanyakazi
wa Halmashauri nchini wamekumbushwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili
waweze kwenda na kasi kubwa katika kuiletea nchi maendeleo.
Rai
hiyo imetolewa jana Mjini Morogoro na Mkurugenzi wa TEHAMA – TAMISEMI,
Erick Kitali alipokuwa anafunga mafunzo ya siku nane yaliyohusu Mfumo
ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa
ujulikanao kama PlanRep.
Kitali
amesema kuwa wafanyakazi wengi wa Halmashauri nchini wamekuwa wakifanya
kazi vile wanavyotaka wao huku baadhi yao wakishindwa kufata utaratibu
uliowekwa lakini kwa sasa wakati huo umepita hivyo kila mmoja anatakiwa
ajitume kwa kuangalia mbele zaidi na kufanya kazi ambayo itabaki kuwa
historia nzuri kwa wananchi.
“Rais
wetu Dkt. Magufuli anajitahidi kuipeleka nchi mbele kimaendeleo na kama
mjuavyo Halmashauri zote ziko chini ya TAMISEMI ofisi ambayo iko chini
ya Ofisi ya Rais hivyo hatutakiwi kumuangusha Mkuu wetu, tunatakiwa
kwenda na kasi zaidi ya aliyokuwa nayo yeye,” alisema Kitali.
Kitali
ameongeza kuwa zamani watu walikuwa wakipelekwa kwenye semina wanafanya
kama sehemu ya kutalii lakini kwa sasa ukipewa mafunzo kama hayo
unakuwa umepewa jukumu ambalo kwa namna moja ama nyingine unatakiwa
ulifanyie kazi.
Aidha,
Kitali amewataka wafanyakazi waliopewa mafunzo ya PlanRep wakayafanyie
kazi kwa kuwapa ujuzi wenzao waliowaacha katika vituo vyao vya kazi ili
kwa pamoja waweze kupanga mipango na bajeti makini kwani siku zote umoja
ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Kwa
upande wake Meneja Mifumo ya TEHAMA – PS3, Revocatus Mtesigwa
amewahakikishia wafanyakazi hao kuwa wameyachukua maoni yao na
watakwenda kuyafanyia kazi kwa ajili ya kuuboresha zaidi mfumo huo.
“Mfumo
sio kitu cha kukamilika kwa siku moja, kila muda unatakiwa uboreshwe
hivyo kwa kuwa nyie ndio mtakaoenda kuutumia na mmetoa mapendekezo mengi
ya kuuboresha zaidi basi mawazo yenu tumeyachukua na tutayafanyia kazi
ili kuleta matokeo mazuri,” alisema Mtesigwa.
Mtesigwa
ametoa rai kwa wafanyakazi waliopewa mafunzo hayo kufanya vizuri katika
Halmashauri zao kwa kuwafundisha wenzao kwa juhudi ili waweze
kuchaguliwa kuwa wawezeshaji watakaokuwa wanatembea nchi nzima
kuwafundisha wengine kwani mradi huo ni mkubwa na bado unahitaji
wawezeshaji wengi.
Mafunzo
haya ya siku 8 yamefadhiliwa na Shirika la Msaada la Marekani (USAID)
pamoja na Serikali ya Tanzania, mafunzo yalihusisha maafisa wa Serikali
wanaotumia mfumo huo wa PlanRep wakiwemo; Waganga Wakuu, Makatibu wa
Afya, Maafisa TEHAMA, Wachumi, Wahasibu na Maafisa Mipango wa Serikali.
0 comments:
Post a Comment