Imeandikwa na John Nditi, Morogoro
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
WAKATI Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
(pichani) akijiandaa kuweka bayana orodha ya viwanda visivyofanya kazi
leo, jana amefanya ziara ya kushtukiza katika viwanda vilivyobinafsishwa
na serikali kwa wawekezaji mkoani Morogoro.
Ziara hiyo aliifanya katika kiwanda cha Moproco, ambako alieleza
kufurahishwa na kasi ya utendaji wake huku akiahidi kutoa taarifa rasmi
kwa viwanda vilivyokiuka agizo la serikali la kushindwa kufanya kazi
miaka 20 tangu vibinafsishwe. Mwishoni wa wiki akiwa mjini Tanga, Rais
John Magufuli alieleza masikitiko yake kuhusu Mwijage kushindwa
kutekeleza maagizo yake ya kumtaka kunyang’anya viwanda vyote
vilivyoshindwa kufanya kazi baada ya kubinafsishwa na kuvirudisha
serikalini. Mwijage ameahidi kuweka kila kitu bayana leo mjini Dodoma.
Kiwanda cha Moproco kimeanza kuajiri wafanyakazi kwa awamu na
kutokana na utendaji huo, waziri huyo alitumia fursa hiyo kuiagiza
mamlaka za ukaguzi kufika kiwandani hapo ili kushauri taratibu
mbalimbali ili zifuatwe. “Nimefika hapa kiwandani kujionea mwenyewe na
nimefurahishwa na hatua ya kiwanda hiki cha Moproco kilivyoanza kufanya
kazi na kuajiri wafanyakazi.
Wamefanya ukarabati wa mashine na hivi sasa uzalishaji wa mafuta
umeanza hapa na hiki ndicho tunachotaka na viwanda vingine vifanye
hivyo,” alieleza Mwijage. Waziri huyo pia alitembelea Kiwanda cha
Morogoro Ceramic Wares Ltd, ambacho ni cha kuzalisha vyombo vya udongo
vya matumizi ya majumbani zikiwemo sahani na vikombe na alikuta hakina
mashine hata moja. Mbali na mashine zake kuondolewa ndani ya kiwanda
hicho, pia alimkuta mlinzi pekee na wamiliki wake wakiwa hawajulikani
walipo, kitendo kilichomchukiza na kueleza kuwa serikali sasa imechoshwa
na hali hiyo.
Baada ya kumaliza ziara yake ya kushitukiza, Mwijage aliondoka eneo
la viwanda la Kihonda na kuahidi kutoa tamko hilo la serikali akiwa
Makao Makuu ya Nchi, Dodoma kuhusu viwanda vitakavyorudishwa serikalini
baada kukiuka agizo la serikali. Naye Mkurugenzi wa Moproco, Talal Abood
alisema uzalishaji huo umeanza mara baada ya kufanyika kwa marekebisho
ya mashine zake zote.
Alisema walianza uzalishaji baada ya kufanya ukarabati mkubwa,
ikiwemo kubadilisha mifumo ya mashine ili kukidhi viwango vya uzalishaji
wa mafuta ya alizeti. Julai mwaka huu wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa
wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, mkurugenzi huyo alisema uzalishaji wa
hatua ya awali ulipangwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu na kutoa ajira za
awali kwa wananchi kati ya 80 hadi 100.
Naye Kebwe ambaye alitembelea kiwanda hicho mapema Julai, alipongeza
jitihada zilizofanywa na uongozi kwa kutekeleza maagizo ya Serikali ya
Awamu ya Tano ya kufufua viwanda vyote vilivyotolewa na serikali.
Akiwa hapo, alifahamishwa kuwa mashine zake zote ziliondolewa na
kupigwa mnada kufidia deni la mkopo wa moja ya benki nchini. Kiwanda
hicho kilichojengwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza kwa ajili ya
kuzalisha vifaa vya majumbani ambavyo ni vyombo vya udongo, masinki ya
maji na vyoo, kilikuwa kinakidhi mahitaji ya ndani kutokana na malighafi
yake kupatikana kwa wingi nchini.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment