Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu
Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari alipokuwa akifungua mafunzo
ya Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya
Serikali za Mitaa ujulikanao kama ‘planRep’. Mafunzo hayo yamefunguliwa
jana Mkoani Morogoro.
Meneja
Mifumo ya TEHAMA kutoka kwenye Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta
za Umma, Revocatus Mtesigwa akizungumza kuhusu malengo ya mafunzo ya
Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za
Mitaa ujulikanao kama ‘planRep’ wakati wa ufunguzi
wa mafunzo hayo jana Mkoani Mororgoro.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO,
Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) unategemewa kuziwezesha halmashauri 93 nchini kufungiwa miundombinu ya
mtandao (Intaneti) ili kuimarisha utendaji kazi wa Halmashauri hizo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari ametoa taarifa hiyo jana mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya Mfumo
ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama planRep.
Tandari
alisema kuwa kutokana na mabadiliko na kurahisishwa kwa teknolojia,
mfumo huo mpya unafanya kazi kwa kutumia mtandao
katika kuwezesha halmashauri nchini kuingiza taarifa za mipango na
bajeti kwa njia ya mtandao kwa hiyo kufungiwa miundombinu ya mtandao
katika halmashauri ni jambo la muhimu na lisiloepukika.
“Kwa
kuwa mradi huu utasaidia kupata mitambo ya Intaneti kwa halmashauri 93
basi natoa angalizo kwa watumiaji wa mfumo huo
kuwa hakutokuwa na kisingizio cha kutokuwepo kwa mtandao bali
tunatarajia matokeo mazuri ya kuongezeka kwa kasi na ari ya kufanya kazi
kwa ufanisi,” alisema Tandari.
Ameongeza
kuwa, kwa Halmashauri ambazo hazitapata fursa ya kufungiwa mitambo hiyo
wajitahidi kutumia vyanzo vya mapato yake
ya ndani kupata fedha za kugharamia ukamilishaji wa mitambo hiyo katika
halmashauri zao kwani bila mitandao itawawia vigumu kutumia mfumo huo
mpya.
Tandari ametoa rai kwa waboreshaji wa mfumo huo kuangalia namna ya kutumia mfumo hata kwa sehemu ambazo kuna changamoto ya
upatikanaji wa intaneti.
Kwa
upande wake Meneja Mifumo ya TEHAMA – PS3, Revocatus Mtesigwa amesema
kuwa mradi huo umesaidia pia katika eneo la uimarishaji
wa miundombinu ya TEHAMA katika ngazi ya mikoa na halmashauri ambapo kwa
kushirikiana na Serikali ilifanyika tathmini ya miundombinu (LAN) na
mifumo ya TEHAMA katika Sekretarieti za Mikoa 13 na halmashauri 93
zilizo chini ya mradi huu.
“Matokeo
ya tathmini hii yaliainisha maeneo yanayohitaji kuboreshwa na tayari
tumeanza kuweka miundombinu hiyo ambapo ifikapo
Agosti 15 mwaka huu, halmashauri zote zilizo chini ya mradi zitakuwa na
mifumo hiyo na ni matumaini yetu kuwa uboreshaji wa mifumo hii utaongeza
ufanisi wa mifumo mingine ikiwemo ya GOT-HOMIS, LGRCIS, EPICOR,
PLANREP, BEMIS na DHIS2,” alisema Mtesigwa.
Mtesigwa
ameongeza kuwa eneo lingine linaloboreshwa ni katika ukusanyaji wa
mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (LGRCIS)
ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo kwa lengo la
kuimarisha na kuboresha ukusanyaji wa mapato katika halmashauri nchini.
Aidha,
kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali mtandao (eGA) pamoja na Ofisi ya
Rais, TAMISEMI, mradi umetengeneza tovuti za
Sekretarieti za mikoa na halmashauri ambazo tayari zimeshaanza kutumika
kwa ajili ya utoaji wa taarifa muhimu na ushirikishwaji wa wananchi.
0 comments:
Post a Comment