Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei.
VIJANA wawili wanaoshikiliwa na Polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za
kumbaka msichana, kumpiga picha za utupu za video na kuzisambaza katika
mitandao ya kijamii, wametajwa kuwa waliweka makazi katika eneo la
Dakawa wilayani Mvomero kwa takribani mwezi kabla ya kufanya kitendo
hicho.
Watuhumiwa hao wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani leo sanjari na
wengi tisa waliosambaza video hiyo, imeelezwa kuwa walifikia kwenye
nyumba ya kulala wageni ya Titii iliyopo kata ya Dakawa na waliishi kwa
muda huo wakijishughulisha na kilimo.
Zuberi Thabiti (30) mkazi wa Mbarali, mkoani Mbeya pamoja Iddy Adamu
(32) mkazi wa Makambako wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka
msichana mwenye umri wa miaka 21, tukio linalodaiwa kufanyika Aprili 28
mwaka huu.
Baadhi ya ndugu wa watuhumiwa tisa wa kusambaza picha za utupu za
msichana huyo , waliliambia gazeti hili kuwa kati ya hao, sita ni ndugu
wa familia moja. Awali, akitoa taarifa jana mjini hapa kwa waandishi wa
habari juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich
Matei alisema uchunguzi na taratibu nyingine zilikuwa zinakamilishwa kwa
ajili ya kufikisha watuhumiwa hao mahakamani leo.
Kamanda Matei alisema msichana huyo aliitwa na Zuberi anayesadikiwa
alikuwa na uhusiano naye kimapenzi ; kwa minajili ya kuangana naye kwa
vile alikuwa akitarajia kurudi kwao Mbarali, mkoani Mbeya .
Alisema kuwa baada ya kuingia chumbani muda mfupi mlango wa chumba
hicho uligongwa kwa nje na Zuberi alikwenda kufungua mlango ndipo
alipomwona Iddy ambaye aliingia ndani akiwa ameshikilia kisu mkononi na
simu.
Kwa mujibu wa kamanda, kabla ya tukio hilo, inadaiwa msichana huyo
kabla ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Zuberi , alishawahi kuwa na
mahusiano kwa nyakati tofauti ya kimapenzi na Iddy bila ya wao
kufahamiana.
Alisema Iddy baaada ya kuingia ndani, alimlazimisha msichana huyo
kufanya mapenzi na Zuberi huku akimrekodi picha za video kupitia simu
yake ya mkononi na baadaye kuzisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya
kijamii.
Kamanda Matei alisema watuhumiwa walimtishia kwa kisu msichana huyo
asipige kelele wakati akifanyiwa kitendo hicho na kumtaka asitoe siri
hiyo vinginevyo atauawa. Baada ya kitendo hicho, imeelezwa kuwa vijana
hao walitoweka na baadaye zilionekana picha za msichana huyo akifanya
ngono na Zuberi.
Inadaiwa baada ya picha hizo za ngono kumfikia mama yake ,
alikazimika kumwita binti yake na kumuuliza na akakiri kufanyiwa vitendo
hivyo kwa kutishiwa maisha yake endapo angetoa siri.
Mama wa msichana hiyo alilazimika kwenda kutoa taarifa Kituo cha
Polisi cha Dakawa , Mei 4, mwaka huu na msako dhidi ya vijana hao
ulifanyika na kukamatwa kila mmoja alikokuwa.
Kamanda Matei alisema kuwa, baadaye picha hizo za ngono zilisambaa
kwenye mitandao ya kijamii na uchunguzi uliofanyika ulifanikisha
kukamatwa kwa watu wengine tisa wa eneo la Dakawa.
Wengine tisa ambao wanakabiliwa na kosa la kusambaza picha za utupu (
Ponografia ) chini ya Kifungu cha 14 (1) (a) cha Sheria ya Makosa ya
Mtandao ya mwaka 2015 ni Rajabu Salehe (26), Said Athuman (26), Musini
Ngai (36), Said Mohamed (24) na Hassan Ramadhan (27).
Wengine ni Ramadhan Ally (26), Lulu Peter (38) na Magreth Njonjome
(30), ambao wote ni wakazi wa kata ya Dakawa, wilayani Mvomero. “
Tumeweza kukamilisha uchunguzi wa awali na kuwakamata watuhumiwa 11 ,
wawili ni waliohusika na vitendo vya ubakaji na wengine tisa kwa
kusambaza picha za video kwenye mitandao ya kijamii na tunawafikisha
mahakamani kesho (leo),” alisema Kamanda Matei.
Kifungu cha 14 (1) cha Sheria hiyo ya Makosa ya Mtandao kinasema
kuwa: “Mtu hatachapisha au kusababisha kuchapishwa kupitia katika mfumo
wa kompyuta- ponografia au ponografia yoyote iliyo ya kisherati au
chafu.
Kifungu cha 14(2) cha Sheria hiyo kinasema: Mtu atakayekiuka Kifungu
kidogo cha ( 1) atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani, atawajibika,
iwapo ni uchapishaji kuhusiana na (a) ponografia, kulipa faini
isiyopungua shilingi milioni ishirini au kutumikia kifungo kwa kipindi
kisichopungua miaka saba au vyote kwa pamoja ; au (b) ponografia iliyo
ya kisherati au chafu, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni
thelathini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka kumi au
vyote kwa pamoja”.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment