ASKARI Polisi Ezekiel Dinoso (32) mkazi wa tarafa ya Mgeta, wilayani
Mvomero mkoani Morogoro amekutwa na noti bandia za Sh 10,000 zenye
thamani ya Sh 870,000, akijiandaa kuzitumbukiza katika akaunti ya
mtandao wa Tigo Pesa katika duka mojawapo eneo la Mawenzi, Manispaa ya
Morogoro.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema jana kuwa
tukio hilo ni la Mei 14, mwaka huu saa 1:00 usiku katika eneo la Mawezi ,
Manispaa ya Morogoro.
Mtuhumiwa alikutwa katika duka la Hadija Hamis (35) mkazi wa
Chamwino, wakati alipohitaji kuwekewa fedha hizo, mwenye duka alimtilia
shaka hivyo kuarifu Polisi. Mtuhumiwa alipokamatwa na askari baada ya
kutolewa taarifa Kituo cha Polisi, alikutwa akiwa na noti bandia 87 za
Sh 10,000.
Alitaja namba za noti hizo ni BX 7287490 zikiwa noti 22 , BX 728792
zikiwa noti 20, BX 728791 noti 19 na BX7287487 zikiwa noti 15 na kufanya
jumla ya thamani ya Sh 870,000 ambazo ni bandia.
Kamanda Matei alisema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na baada ya uchunguzi kukamilika atafikishwa mahakamani.
Katika tukio jingine, Rashidi Shabani (30) na Michael Lukasa (39),
wote wakazi wa Ngerengere wanashikiliwa na Polisi kwa kuwakuta na nyama
ya nyati kilo 300 na silaha aina ya gobole iliyotumika kumuulia mnyama
huyo.
Kamanda wa Polisi wa Morogoro, Matei, alisema walikamatwa Mei 14,
mwaka huu saa 2:00 usiku katika kijiji cha Kinonko, kata ya Gwata,
wilaya ya Morogoro. Matei alisema, kukamatwa kwa watuhumiwa hao
kumetokana na jitihada zinazofanywa na polisi kwa kushirikiana na
wananchi katika kukomesha vitendo vya uhalifu.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment