WATU watatu wakiwemo waendesha bodaboda wawili wamenusurika kifo
baada ya kupata kipigo kutoka kwa wananchi wakituhumiwa kupora mkoba wa
mwanamke.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema tukio
hilo ni la juzi saa moja asubuhi katika eneo la Msamvu, Manispaa ya
Morogoro.
Kamanda Matei alitaja waliotambulika kwa jina moja moja ni
Makhirikhiri (mwendesha pikipiki) na Ngasa ambao wote ni wakazi wa
Misufini. Mwingine hakutambuliwa mara moja.
Alisema wakiwa na pikipiki yenye namba za usajili MC 436 AVX aina ya
Sanlg, walipora mkoba wa Pendo Wilson (30), mkazi wa Msamvu akiwa njiani
kwenda kazini kwake.
Alisema mwanamke huyo alipiga kelele za kuomba msaada na ndipo watu
walioshuhudia tukio, walianza kufuatilia vijana hao kwa pikipiki na
kuwakamata walipofika maeneo ya Modeco-Ipoipo.
Kamanda Matei alisema wananchi wenye hasira walianza kushambulia kwa
magongo na mawe na kuwasababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili.
Watuhumiwa hao waliokolewa na polisi waliofika eneo la tukio baada ya
kupata taarifa za tukio. Waliwahishwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Morogoro kupata matibabu.
Kufuatia vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na madereva bodaboda,
Kamanda Matei alisema polisi itaendelea kusaka wahalifu ambao baadhi yao
wanatoka nje ya mkoa na kujihusisha na biashara za bodaboda, lakini
wakijihusisha na matukio ya uhalifu.
Amewataka viongozi wa vyama vya waendesha bodaboda kukagua wanachama
wao kwa kuwasajili watambulike maeneo wanayofanyia kazi zao na iwe
rahisi kuwatambua. Alitoa mwito kwa wananchi kuacha tabia ya
kujichukulia sheria mkononi wanapowakamata wahalifu ni vyema watoe
taarifa polisi.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment