Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameeleza kuwa
Serikali inatoa kipaumbele katika uchimbaji wa madini ya graphite nchini
kutokana na umuhimu wake duniani ikiwemo kutumika kama malighafi ya
kutengenezea betri za simu, kalamu za risasi na kompyuta mpakato.
Aliyasema hayo wakati alipokutana na Kampuni ya Tanzgraphite (TZ)
ambayo ni kampuni tanzu ya Kibaran Resources inayofanya utafiti wa
madini hayo tangu mwaka 2012 eneo la Epanko wilaya ya Ulanga, Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, Profesa Muhongo alisema madini
hayo yana soko kubwa duniani kwani hutumika pia katika utengenezaji wa
vilainishi mbalimbali. Profesa Muhongo alitoa kauli hiyo baada ya
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Jacka Mwambi kumueleza kuwa kampuni
hiyo imepanga kuanza uzalishaji wa madini hayo mwaka 2017 lakini ili
kutekeleza hilo kwa ufanisi, wanahitaji msaada serikalini ikiwemo wa
ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme cha Ifakara kitakachowasaidia kupata
umeme wa uhakika katika eneo la uzalishaji.
Mwambi alisema pia wanaiomba serikali kukamilisha ujenzi wa daraja
litakalokatisha mto Kilombero ambalo litawapa uhakika wa usafirishaji wa
madini hayo tofauti na kivuko kinachotumika sasa.
“Changamoto nyingine ni baadhi ya wananchi wanaozunguka eneo hilo la
uchimbaji ambao wanaonekana kutokukubaliana na mradi kufanyika katika
eneo husika, tumejaribu kujadiliana nao kwa kuhusisha ngazi mbalimbali
za uongozi lakini bado kuna changamoto ya mawasiliano chanya kati ya
kampuni na wananchi,” alisema Mwambi.
Akizungumzia uchimbaji wa madini ya graphite duniani, Mwambi alisema
kwa sasa nchi za China, Brazil na India ndizo zinaongoza kwa usambazaji
wa madini hayo ambazo wanazalisha tani milioni 1.2 kwa mwaka.
Alisema kwa Afrika, Msumbiji imeonekana kuwa na mashapo mengi na
kueleza kuwa endapo Tanzania itafanikiwa kuchimba madini hayo katika
eneo la Epanko, itaifanya kuwa mzalishaji mkubwa wa madini hayo barani
Afrika.
Alisema gharama ya uendeshaji wa mradi huo wa Epanko itakuwa ni Dola
za Marekani milioni 77.5 na uhai wa mgodi unatarajiwa kuwa miaka 25.
Alisema faida zitakazotokana na uzalishaji wa madini hayo wilayani
Ulanga ni pamoja na ajira 1,500 za moja kwa moja huku akieleza kuwa
ajira zisizo za moja kwa moja zitaongezeka mara sita zaidi ya zile za
moja kwa moja, pia wafanyakazi katika kampuni hiyo wenye ujuzi na wasio
na ujuzi watapatiwa mafunzo ya kuwaendeleza.
Kuhusu changamoto ya wananchi kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo,
Profesa Muhongo ametuma timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na
Madini kwenda katika eneo hilo kuzifahamu changamoto hizo kwa undani na
kuwasilisha kwake ripoti keshokutwa saa nne asubuhi.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment