Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
akiwa kwenye wadi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro
SERIKALI ya Awamu ya Tano imejipanga kutatua changamoto za
upatikanaji wa dawa katika hospitali zake nchini kwa kuongeza bajeti ya
dawa na vitendanishi kutoka bajeti ya Sh bilioni 70 mwaka uliopita hadi
kufikia Sh bilioni 350 kwa mwaka 2016/2017.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
alisema hayo juzi wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Morogoro.
Ummy alisema kuwa lengo la kuongeza bajeti hiyo ni kuhakikisha kuwa
huduma za afya katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya
zinapatikana kwa uhakika ili kuwapunguzia wananchi changamoto za ukosefu
wa dawa na vifaa tiba wakati wanapokwenda kupata huduma.
“Naomba bajeti hiyo ipitishwe na Bunge ili kuwezesha upatikanaji wa
dawa kwa uhakika katika hospitali za serikali nchini,” alisema Ummy.
Hivyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa sekta ya afya
kujenga mahusiano mazuri na wananchi pindi wanapokwenda kupata huduma
ili huduma wanazozitoa ziendane na viapo vya utumishi wao ili kuepuka
hali ya sintofahamu iliyoibuka siku za hivi karibuni ambapo madaktari na
wauguzi kupigwa na wananchi katika maeneo ya kazi.
Pamoja na hayo, alimwomba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven
kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa kwa lengo la kuwahakikishia
usalama wauguzi, madaktari wanaotishiwa maisha na baadhi ya ndugu wa
wagonjwa ili pande zote mbili ziwe katika hali ya usalama na kunufaika
na huduma za matibabu bila ya vikwazo.
Pia aliwataka watendaji na watumishi katika hospitali na vituo vya
afya kuwa wawazi kwa kuweka matangazo kwenye mbao za matangazo juu ya
gharama halisi za vipimo au upasuaji ili wananchi wajue gharama halisi.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro Dk Rita Lyamuya, alisema kuwa hospitali hiyo imefanikiwa
kuongeza mapato yake katika duka la dawa kutoka mtaji wa Sh milioni tano
hadi milioni 120 licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za
uchakavu wa majengo na miundombinu yake.
Dk Lyamuya alisema kuwa mbali na mafanikio hayo , Hospitali ya mkoa
ilishika nafasi ya pili kwa usafi katika hospitali za rufaa hapa nchini
na uboreshaji wa huduma za afya kwa wazee kwa kuanzisha dawati maalumu
limepewa jukumu la kushauri na kuwahudumia wazee wanapofika hospitalini
kupata huduma.
Alisema, pamoja na mafanikio hayo, zipo changamoto mbalimbali hususan
ukosefu wa watumishi 75, akiwemo daktari bingwa wa macho, uchakavu wa
chumba cha kuhifadhi maiti, majokovu, uzio wa hospitali na ufinyu wa
bajeti ya uendeshaji na kutokuwepo kwa mtaalamu wa Tehama.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment