MWILI wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), Amatus Liyumba aliyefariki juzi jijini Dar es Salaam
unatarajiwa kusafirishwa kwenda kuzikwa kijijini kwake Mahenge mkoani
Morogoro.
Liyumba alifariki dunia juzi saa 10 jioni katika Hospitali ya Agha
Khan jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya
kisukari na shinikizo la damu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji wa familia hiyo, Moses
Liyumba alisema mipango ya mazishi inaendelea kufanyika nyumbani kwa
marehemu maeneo ya Triple Seven, Mikocheni, Dar es Salaam na huenda leo
au kesho mwili wa marehemu ukasafirishwa kwenda kijiji cha Vigoi kwa
maziko.
“Tunaendelea na taratibu mbalimbali za mazishi na huenda mambo
yakienda sawa kesho (leo) au kesho kutwa tukausafirisha mwili wa
marehemu hadi kijijini kwake kwa maziko,” alisema Liyumba.
Kwa mujibu msemaji huyo wa familia, marehemu ameacha watoto wanane
ambao walizaliwa na mama tofauti kati yao wa kike sita na wa kiume
wawili.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment