Home » » Mvua yaacha 5,000 bila makazi Kilosa

Mvua yaacha 5,000 bila makazi Kilosa

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Imeandikwa na John Nditi, Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Kebwe Steven Kebwe.
MAFURIKO yameziathiri kaya 1,238 zenye idadi ya watu 4,765, kubomoa nyumba 144 na nyingine 1,120 kuharibiwa kutokana na kuzingirwa na maji ya mvua katika vijiji vitano vilivyopo Kata ya Msowero, Tindiga na Masanze wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu kutoka Kilosa juzi jioni, Mkuu wa Wilaya hiyo, John Henjewele alisema taarifa za mwisho alizozikusanya kuhusu mafuriko ya mvua za masika zilizokuwa zimeanza kunyesha tangu Aprili 23, mwaka huu maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, kuwa vijiji vitano vilivyopo kata tatu, wananchi wake wameathiriwa na mafuriko hayo yaliyoharibu mazao na nyumba za kuishi.
Alivitaja vijiji hivyo na kata zake kwenye mabano ni Mambegwa (Msowero), Malui na Changalawe (Masanze) Tindiga A na B katika Kata ya Tindiga. Kaya 1,238 zenye idadi ya watu 4,765 zimeathirika wakati nyumba 1,120 zimeharibiwa na kuzingirwa na maji, na nyumba 144 zimebomoka.
Aliyataja madhara mengine ni visima 18 kuharibiwa na mvua hizo, vyoo katika nyumba zimejaa maji na kufurika, sambamba na soko la Tindiga kuingiliwa na maji, pamoja na ofisi za watendaji wa Kata ya Masanze na Tindiga, mashamba ya mazao kujaa maji na kufunikwa na mchanga.
Alisema kutokana na mafuriko hayo, barabara ya Kilosa- Mikumi haipitiki kwa sasa, kwa kuwa imeharibiwa vibaya na maji ya mvua hizo; lakini hakuna madhara ya kibinadamu kwa vile jamii ya Kilosa hasa yenye kukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara imejengewa mpango wa utayari wa kukabiliana na majanga hayo.
Nao wananchi wa Kijiji cha Changalawe Kata ya Masanze waliiomba Serikali kuwapatia msaada wa dharura wa chakula, makazi ya muda na mbegu za mahindi ya muda mfupi ili kupanda upya kutokana na zaidi ya ekari 1,000 za mazao kuharibiwa na mafuriko ya mvua.
Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Joseph Haule maarufu Profesa Jay, aliwatembelea wananchi hao na kueleza kuwa anafanya jitihada za haraka kuhakikisha wanapata msaada wa hifadhi.
Chanzo Gazeti la Habari leo

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa