Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina.
Rungu la faini kutokana na ukiukwaji wa sheria za mazingira limeendelea kuviandama viwanda mbalimbali vya mkoa wa Morogoro.
Hivi sasa viwanda vya sukari vya Mtibwa na Ilovo kilichoko
Kilombero pamoja na kile cha kutengeneza ngozi cha ACE, vimetozwa jumla
ya sh. milioni 40 kwa makosa ya aina hiyo katika maeneo yao.
Uamuzi huo ulitolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina, akiwa katika mwendelezo wa
ziara yake mkoani hapa akiambatana na maofisa wa Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc).
Kiwanda cha Ilovo kimetozwa faini ya sh. m,ilioni 25 baada ya
kubainika kuwa na mfumo mbovu wa utunzaji taka ngumu na kushindwa
kuhifadhi vyema mabaki ya mabati yanayotolewa kiwandani hapo. Mbali na
faini ambayo inatakiwa kulipwa ndani ya siku saba, walitakiwa
kurekebisha upungufu huo ndani ya siku 30.
Naibu waziri huyo aliutaka uongozi huo kuhakikisha upungufu 40
uliotajwa kwenye ripoti ya ukaguzi, iliyofanywa na Nemc zaidi ya miezi
mitatu iliyopita, unafanyiwa marekebisho sambamba na kuutolea taarifa
uwanja wa ndege ulioko ndani ya kiwanda hicho ambao hauna cheti chochote
cha ukaguzi.
Kwa upande wa kiwanda cha ngozi cha ACE cha mjini Morogoro,
serikali imekitoza faini ya Sh. milioni 15 kutokana na kubainika kuwa na
mfumo mbovu wa utiririshaji na uhifadhi wa maji taka.
Mpina pia aliiagiza menejimenti ya kiwanda kudhibiti harufu mbaya
inayolalamikiwa na wananchi, hususan walio jirani na kiwanda hicho.
Naibu Waziri Mpina alifanya ziara pia katika soko kuu la mjini
Morogoro na kuagiza ujenzi mpya wa soko kuzingatia vizimba vya uhifadhi
wa taka ili zisitawanyike na kuutaka uongozi wa manispaa kutofanya
mlundikano wa taka katika eneo hilo kama ilivyoonekana.
Ziara hiyo ya Mpina iliyafikia pia maeneo ya kituo kikuu cha mabasi
cha Msamvu, kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kula cha Abood (Moproco),
Kiwanda cha maturubai, Kiwanda cha nguo cha 21st Century, Kiwanda cha
Magunia na mabwawa yanayopokea majitaka yatokayo viwandani.
Kutokana na maagizo ya Naibu Waziri, mtaalamu wa mazingira kutoka
Ilovo, Mary Kigula, alisema watahakikisha wanatekeleza ikiwa pamoja na
kupanda miti na kutoa huduma za kijamii katika maeneo yanayowazunguka.
Naye Mkuu wa Idara ya Uzingatiaji wa Sheria ya mazingira kutoka
Nemc, Alfred Msokwa, alisema baraza limekuwa likitoa ushauri na
maelekezo kwa uongozi wa viwanda lakini wengi wamekuwa wakipuuza.
Msokwa alisema tangu mwaka 2013 NEMC imefanya ukaguzi katika
viwanda takribani vyote mkoani Morogoro na kutoa ushauri ambapo baadhi
ya viwanda bado vipo katika utekelezaji wa marekebisho yake huku vingine
vikipuuzia maelekezo hayo na kujikuta vikitakiwa kulipa faini kwa
mujibu wa sheria.
CHANZO:
NIPASH.
0 comments:
Post a Comment