WIZARA ya Viwanda na
Biashara, imejitosa rasmi kupambana na watu wanaoingiza sukari ya
magendo na kusababisha viwanda vya sukari nchini kuanza kupunguza
uzalishaji.
Pia Wizara hiyo imesema mapambano yatafanywa kupitia doria endelevu kwa kushirikisha Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ili kuhakikisha wanaoingiza sukari hiyo wanadhibitiwa.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Janeth Mbene, alitangaza hatua hiyo juzi mkoani Kilimanjaro alipofanya ziara kwenye Kiwanda cha Kuzalisha Sukari cha (TPC) kilichopo Wilaya ya Moshi ili kujionea uzalishaji wa sukari unavyoendelea.
Alisema ni jambo la aibu kwa baadhi ya Watanzania kuendelea kuingiza sukari kwa njia ya magendo nchini na kusababisha viwanda vya ndani kupoteza soko.
Aliongeza kuwa, mbali ya viwanda hivyo kupoteza soko; pia ajira nyingi za Watanzania zipo mashakani kwani uzalishaji wa sukari umeshuka kwa kiwango kikubwa.
Mbene alisema, Serikali haipo tayari kuona zaidi ya Watanzania 4,000 wakipoteza ajira kwenye kiwanda hicho ambacho uzalishaji wake umeshuka kutokana na uingizwaji wa sukari ya magendo kutoka nje ya nchi bila kutozwa kodi.
"Hatua hii inawakatisha tamaa wawekezaji wa viwanda vya ndani, wanaoingiza sukari za magendo huwa hawalipi kodi ikilinganishwa na wanaozalisha sukari nchini," alisema.
Alisema Serikali ina mkono mrefu hivyo wanaojishughulisha na biashara ya magendo watashughulikiwa bila kuonewa huruma ili kulinda viwanda vya ndani, ajira za Watanzania na uchumi.
"Ni wazi kuwa, wanaoingiza sukari za magendo nchini majina yao yanafahamika hivyo kitakachofanyika ni kuwafuatilia kwa kina kupitia doria endelevu waweze kuchukuliwa hatua.
"Naombeni muda, jambo hili nitalifikisha kwa wenzangu, ninaamini litafanyiwa kazi haraka, kwanza linaigusa Wizara yangu, sipo tayari kuona viwanda vya ndani vinakufa; nataka viendelee kustawi ili kukuza na kuinua uchumi wetu," alisema.
Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPC, Robert Baissac, alisema uzalishaji kiwandani hapo umeshuka kwa kiwango kikubwa kutokana na kukosa soko.
Alisema hali hiyo imesababisha badala ya kuzalisha tani 420,000 kwa mwaka, uzalishaji umeshuka hadi tani 320,000 kutokana na uingizaji sukari kutoka nje ya nchi ambazo zinauzwa bei nafuu hivyo wao kukosa soko.
"Mahitaji ni tani 420,000 kwa mwaka lakini uzalishaji umeshuka hadi tani 320,000...kuna upungufu wa tani 100,000 jambo ambalo linaathiri uchumi wa nchi na gharama za uendeshaji," alisema na kuongeza kuwa, ajira na mishahara ya wafanyakazi pia wanalazimika kupunguza.
Hivi karibuni, baadhi ya viongozi waandamizi serikalini walituhumiwa kujihusisha na sakata la kuingiza sukari ya magendo na wengine wakisema ikibainika wanahusika na jambo hilo watakuwa tayari kujiuzulu nyadhifu
Chanzo:Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment