CHUO Kikuu Mzumbe kimeanzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Tampere
cha nchini Finland kufanya utafiti utakaosaidia kujenga uwezo na hali
bora ya maisha katika kaya nchini Tanzania.
Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Josephat Itika, alisema
ushirikiano huo unalenga kuja na majibu ya kuboresha hali ya maisha ya
kaya Tanzania.
Profesa Itika alikuwa akizungumza wakati wa mahafali ya 13 ya chuo hicho mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.
“Utafiti huu unalenga kuboresha hali ya maisha ya kaya kutokana na
ukweli kwamba kuna tatizo la umasikini katika kaya zetu,”alisema.
Alisema utafiti huo utakuja na mbinu mpya itakayosaidia kuleta
ufumbuzi juu ya suala la umasikini katika kaya, ili kuondokana nao.
Inatarajiwa kwamba utakapokamilika, utafiti huo utapelekwa kwa wadau
mbalimbali ikiwemo serikali, ili hatua za makusudi ziweze kuchukuliwa.
Alifafanua kwamba kaya zikiwa na maisha mazuri, ni kiashiria kikubwa
kwamba vipato vya jamii vimekua na kukua huko hujenga uchumi wa nchi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Mzumbe imekuwa ikizidisha ushirikiano
na vyuo vya nje, ili kujijengea uwezo katika maeneo ya ufundishaji,
utafiti na huduma za ushauri.
Miongoni mwa vyuo ambavyo chuo hicho kimeanzisha ushirikiano ni
pamoja na Chuo Kikuu cha London kupitia Idara ya Mafunzo ya ualimu na
chuo Kikuu cha CMR Bangalore, India kupitia kampasi ya Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Profesa Daniel Mkude alisema chuo
kimeanza kupata maendeleo makubwa kutokana na ufundishaji wa utumiaji
njia ya kietroniki.
Alisema pia wanafunzi wanafundishwa jinsi ya kutumia Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu
fani zao.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa chuo, Utawala na Fedha, Profesa Faustin
Kamuzora aliwataka wahitimu hao kuzingatia weledi na maarifa katika
utendaji kazi kwenye sekta ya umma au binafsi.
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 2125 walitunukiwa; kati ya hao, wanawake wakiwa 922 na wanaume 1174.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment