Home » » MASHAMBA YA BANGI YATEKETEZWA MORO

MASHAMBA YA BANGI YATEKETEZWA MORO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

OPERESHENI maalumu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kutokomeza mashamba ya bangi imefanyika na kufanikiwa kuwakamata watu wanne wamiliki wa mashamba hayo katika Wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro.
Jeshi hilo katika oparesheni yake, limefanikiwa pia kuteketeza mashamba matano ya bangi huku wakiendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaodaiwa kumiliki mashamba hayo.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paul, alisema uteketezaji wa mashamba hayo ulifanyika Oktoba 26 kutokana na kuwepo kwa matukio mbalimbali ya ukamataji wa bangi katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Aliwataja walioshikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumiliki mashamba hayo kuwa ni Tekra Andrea (44), Ferdinand Mlovosa (62), Alex Gilbert (42), na Erasto Sanga (28), wote wakiwa ni wakazi wa Chabima wilayani Kilosa.
Alisema kuwa watu hao wanne wanatuhumiwa kumiliki ekari tatu za mashamba ya bangi sambamba na kukutwa na bangi kilo 20 zilizokuwa zimeanikwa katika mashamba hayo.
Aidha, aliwataja wanaotafutwa na polisi kuwa ni Gasper Athumani mkazi wa Kungwe tarafa ya Mkuyuni Wilaya ya Morogoro, ambaye anadaiwa kumiliki ekari moja ya shamba la bangi katika msitu wa Kungwe na Ngova Kikono mkazi wa Masalawe tarafa ya Mgeta, Mvomero.
Kamanda Paul, alisema watuhumiwa wanne waliokamatwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote  mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Aidha, aliwaomba wananchi kusaidia jeshi la polisi kuwafichua wale wote wanaodaiwa kumiliki mashamba mahali popote mkoani hapa hata kama ni mbali, jeshi hilo litafika kwa ajili ya uteketezaji.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa