Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JESHI la Magereza nchini limeikabidhi shule ya Sekondari Bwawani basi lenye thamani ya sh milioni 120 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za gharama ya usafiri na juhudi ya kukuza elimu katika shule hiyo iliyoko mpakani mwa Mkoa wa Pwani na Morogoro.
Akikabidhi basi hilo kwenye tafrija fupi iliyokwenda sambamba na mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne shuleni hapo hivi karibuni, Kamishna Jenerali (CGP), John Minja, mbali na kutimiza ahadi hiyo aliyoitoa mwaka jana, alibainisha kuwa jeshi linakusudia kuifanya shule hiyo kuwa kitovu cha wataalamu katika fani mbalimbali zenye tija katika taifa.
CGP Minja, alisema jeshi limejipanga kuzikabili changamoto zilizopo, ikiwemo kuondoa tatizo la maji kwa kununua mashine na pampu itakayovuta na kusukuma kwenye birika litakalokuwa likiyasambaza shuleni hapo.
Awali, Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Kamishina wa Utawala na Fedha wa Jeshi hilo, Gaston Sanga na Makamu Mkuu wa shule, Emmanuel Lwinga wakitoa shukrani kwa utekelezwaji wa ahadi hizo, walitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwemo uzio, upungufu wa walimu na utoro kwa baadhi ya wanafunzi.
Waliwaomba wadau wa elimu, kuchangia maendeleo ya shule hiyo ili kuliwezesha taifa kupata viongozi wenye moyo na ari ya kuwatumikia na kulikwamua taifa na changamoto ya umasikini.
Baadhi ya wahitimu, waliliomba jeshi hilo kuanzisha utaratibu wa kuandaa vijana watakaolitumikia badala ya kusubiri kupitia utaratibu wa kawaida, kwa kuwa unasababisha kupata watumishi wasio na malezi ya uadilifu kazini.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment