SERIKALI ya Mkoa wa Morogoro na wadau wengineo wametoa misaada mbalimbali zikiwemo fedha tasilimu kwa majeruhi wa ajali ya basi kugonga treni wanaotibiwa hospitali ya Mt. Francis wilayani hapa.
Katika misaada hiyo, ofisi ya mkuu wa mkoa imetoa kwa majeruhi 14 sh 50,000 kila mmoja huku majeruhi mmoja ambaye hali yake haikuwa nzuri akipewa sh 200,000 ili zimsaidie kuhamishiwa hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Mbali na fedha, misaada mingine ni pamoja na maji ya kunywa, sabuni za miche na karatasi za maliwato (toilet paper).
Akikabidhi fedha hizo, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Eliya Ntandu, alisema mkoa umesikitishwa kutokea kwa ajali hiyo huku akiendelea kusisitiza kuwa mpango wa serikali ni kutokomeza kabisa ajali za vyombo vya moto kwa madereva kuelimishwa juu ya usalama barabarani.
Mdau mwingine aliyetoa msaada ni Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, ambaye aliwataka wananchi wengine kujitokeza kuwasaidia majeruhi walioendelea kulazwa katika hospitali hiyo, kwani wengi wao inaonekana wametoka nje ya Ifakara.
Awali, Ofisa Uhusiano wa hospitali ya Mt. Francis, Nestory Mlagani, alisema hadi sasa chumba cha maiti umebaki mwili mmoja kati ya 11.
Ajali hiyo ilitokea wiki iliyopita ikihusisha basi la kampuni ya Al Jabry linalofanya safari zake kati ya Morogoro na Ifakara kuigonga treni ya Tazara maeneo ya Kiberege na kusababisha vifo vya watu 12 huku wengine zaidi ya 30 wakijeruhiwa, ambako dereva wa basi hilo alikimbia baada ya kusababisha ajali hiyo.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment