Home » » MADIWANI WAKERWA UCHAKACHUAJI WA TUMBAKU

MADIWANI WAKERWA UCHAKACHUAJI WA TUMBAKU

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, wameelezea masikitiko yao kuhusu uchafuzi wa tumbaku unaofanywa na baadhi ya wakulima wasio waaminifu na kutaka itungwe sheria kukabiliana na uovu huo.
Walitoa rai hiyo baada ya kutembelea kiwanda cha kusindika tumbaku cha Morogoro (TTPL), mwishoni mwa wiki ambapo ujumbe huo ulijumuisha madiwani 26 na maofisa 10 kutoka wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Uyui, Saidi Ntahondi, alisema ziara hiyo imetoa mwanga jinsi kiwanda kinavyofanya kazi kwa teknolojia na nidhamu ya kikazi.
Alisema changamoto kubwa inayovikumba viwanda vya kusindika tumbaku nchini ni vitendo vya makusudi vya kuongeza vitu visivyohusika na tumbaku (NTRM), jambo linalofanywa na wakulima wasio waaminifu kwa lengo la kuongeza uzito wa zao lao.
"Baraza langu litafanya kazi kwa kuandaa sheria ndogo ndogo kudhibiti tabia hiyo na wakulima watakaoendelea na mchezo huo watasimamishwa," alisema Ntahondi.
Maofisa wa TTPL, waliwaonyesha madiwani baadhi ya NTRM zilizoongezwa kwenye majani ya tumbaku yakiwamo mawe, mifuko ya plastiki na chupa, ikiwa ni baadhi tu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora, Anselim Teendwa, alisema kuwa hali hiyo itaharibu sifa ya Tanzania katika soko la dunia, kwani karibu asilimia 95 ya zao hilo husafirishwa nje ya nchi.
Naye Meneja wa TTPL, Jimmy Mollel, akiwa ameambatana na msaidizi wake, Ambrose Mtena, waliwaomba madiwani kuwahamasisha wakulima juu ya umuhimu wa uzalishaji wa majani ya tumbaku yenye viwango bora.
Kwa niaba ya wenzao, madiwani wa viti maalum, Janet Mgumia na Elizabeth Kandoro, walieleza kufurahishwa na ajira za wanawake katika viwanda vya msingi vya usindikaji tumbaku.
TTPL ambacho awali kilimilikiwa na serikali kabla ya kubinafsishwa, sasa ni moja ya kiwanda kinachotoa ajira kubwa mkoani Morogoro kikiajiri zaidi ya watu 2,500 ambako kati yao, 200 wana ajira za kudumu na waliobaki 2,300 ajira za msimu.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa