Home » » WATOTO WALEMAVU WASAIDIWA BAISKELI

WATOTO WALEMAVU WASAIDIWA BAISKELI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, Furaha Lilongeri, akiwa anamweka sawa mtoto mlemavu, Magdalena Ngwira, kwa ajili ya kukaa kwenye baiskeli maalum ya walemavu zilizotolewa msaada na 

Watoto wenye ulemavu katika kata ya Mahenge, wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, wamepatiwa msaada wa baiskeli 30 maalum za walemavu.

Msaada wa baiskeli hizo ambazo zimetengenezwa maalumu kwa watoto wanaoishi vijijini, umetolewa na kampuni ya Kibaran Resources inayojihusisha na utafiti wa uchimbaji wa madini ya Uno kwenye kijiji cha Epanko, wilayani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi baiskeli hizo mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa kampuni ya Kibaran Resources Tanzania, Grant Pierce, alisema  msaada huo ni sehemu ya miradi ya maendeleo ya kijamii ambayo kampuni hiyo imeazimia kuifanya ili kuwa karibu na jamiii inayowazunguka.

“Msaada huu ni sehemu ya azimio tuliloweka la kuwekeza katika jamii zinazotuzunguka. Watu wanaoishi na ulemavu husahaulika katika jamii na hawapati haki zote zinazostahili kwa binadamu. Haki za binadamu ni sawa kwa watu wote bila kujali hali zao,” alisema na kuongeza: 

“Kukosa uwezo wa kujihudumia mwenyewe huleta mateso kwa binadamu hasa watoto. Tunafurahi kuwasaidia watoto katika jamii hii kwa kuwapa uwezo wa kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine kwa urahisi na tunaamini itasaidia kuboresha maisha yao ya kila siku.”

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ulanga, Furaha Lilongeri, akimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo,Francis Miti, alisema amefurahishwa na moyo wa kampuni  hiyo wa kujali jamii inayoizunguka haswa kundi hilo la walemavu.

Alisema msaada huo utawawezesha watoto hao kushiriki shughuli mbalimbali katika jamii pamoja na kufikia malengo yao, kama vile kwenda shule kama watoto wengine ili kujipatia elimu ambayo ni msingi wa maisha yao.

Wakizungumza kwa niaba ya watoto wao, walezi wa watoto waliopewa baiskeli hizo walitoa shukurani kwa uongozi wa kampuni ya Kibaran Resources kwa kuwasaidia watoto wao kutimiza ndoto zao za kushiriki katika fursa zilizopo kwenye jamii sawa na watoto wengine wasio na ulemavu. 
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa