Home » » WAKAZI WA KISWIRA WAPEWA ELIMU UONGEZAJI THAMANI MAZAO

WAKAZI WA KISWIRA WAPEWA ELIMU UONGEZAJI THAMANI MAZAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

CHUO cha Maendeleo ya Wananchi Bigwa mkoani hapa kimeendesha mafunzo ya matumizi ya nishati ya jua katika uhifadhi na uongezaji thamani mazao kwa wakazi wa Kijiji cha Kiswira, Kata ya Matombo.
Wakazi hao, kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na tatizo la uhifadhi na uongezaji thamani kwa mazao ya msimu kama vile mboga na matunda.
Katika mafunzo hayo ya wiki moja yaliyofungwa hivi karibuni na na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro, Humphrey Mbita, yalidhaminiwa na shirika la REYA na kushirikisha washiriki 20 wakiwemo wanawake 18.
Baadhi ya wahitimu akiwemo Constantine Chewe, Maria Patrick na Cecilia Chuma, kwa nyakati tofauti walisema mafunzo hayo yamewawezesha kupata mbinu rahisi ya kuhifadhi mazao hayo na kuyauza wakati mwingine kwa bei nzuri.
"Elimu hii itatusaidia kupunguza tatizo la matunda na mboga mboga kuharibika kwa kukosa soko, kwani sasa tuna uhakika wa kuuza mazao haya muda wowote, iwe ni wa msimu wa mazao au vinginevyo," alisema Constantine.
Naye Mkuu wa chuo hicho, Peter Maongezi, aliomba wadau mbalimbali nchini kujitokeza kukidhamini chuo hicho, ili kiongeze ufanisi na lengo lake la kuibadili jamii katika kutumia rasilimali zilizopo kujiendeleza.
Kwa upande wake mgeni rasmi Mbita, aliwataka wahitimu hao kutumia vizuri ujuzi walioupata kwa manufaa ya jamii, kutobweteka na kuridhika na elimu waliyoipata, badala yake wajiendeleze zaidi ili kujiongezea ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kuwainua kiuchumi.
Mkoa wa Morogoro ni kati ya mikoa inayozalisha matunda na mboga mboga kama vile karoti, soya, lozera, majani ya kunde na mboga za asili kama chunga na hombo kwa wingi na yamekuwa hayana tija kwa wazalishaji.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa