Home » » HOFU YATANDA CHUO KIKUU CHA ST. FRANCIS

HOFU YATANDA CHUO KIKUU CHA ST. FRANCIS

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WANACHUO zaidi ya 500 wa shahada ya udaktari katika chuo kikuu cha afya cha St. Francis Ifakara, Kilombero mkoani Morogoro wako kwenye hofu ya kufukuzwa baada ya kupandishwa ghafla gharama za chuo ikiwemo ada iliyopanda kutoka sh milioni 2 hadi milioni 3.6 na kutakiwa kulipa kwa muda mfupi.
Hofu hiyo imeibuka kutokana na tangazo la mkuu wa chuo hicho, Prof. Cassian Magori, la Septemba 10 mwaka huu, kuwataka wanachuo bila kujali udhamini wake chuoni hapo kulipa tasilimu kiasi hicho au wanaolipiwa na bodi ya mikopo nchini (TCU), kumwandikia barua inayoelekeza chuo kukata fedha za kujikimu.
Mbali na kupanda kwa ada na kutakiwa kuwa imelipwa ndani ya mwezi mmoja, pia tangazo hilo linaonyesha gharama nyingine zikiwemo za hosteli kupanda kutoka sh 140,000 hadi 250,000 usajili kwa bweni sh 340,000 hadi 1,000,000 na nyingine zinazofanya jumla ya gharama chuoni hapo kuzidi sh milioni 7.2.
Hata hivyo, uongozi akiwemo mkuu wa chuo, Prof. Magori na Ofisa Mikopo ambaye pia ni mrajisi, Rosemary Mhila, hawakutaka kutoa ushirikiano kwa mwandishi wa habari hizi badala yake walimjibu kwa mkato na kumtisha.
“Jambo hilo tumeshalimaliza, kwa hiyo sio ‘issue’ tena niache mimi nina kazi nyingi za kufanya hapa,” Prof. Magori alisema kwa mkato.
Awali alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya mikopo kwa wanachuo chuoni hapo na kama bodi ya mikopo TCU ina taarifa juu ongezeko la gharama chuoni hapo, Mhila alimkatisha mwandishi wa habari hizi akimtaka asimzoee na maswali yake ya kipuuzi.
“Usinizoee kama familia yako. Aliyekuelekeza na wewe ni wapuuzi tena sana…tumia akili kama baba wa familia,” alijibu Mhila kwa ujumbe wa simu ya mkononi.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao, baadhi ya wanachuo walisema uongozi unaendesha mambo kibabe na kienyeji bila kujali sheria na taratibu hasa za mikopo, ikizingatiwa wengi wa chuoni hapo wanagharimiwa na serikali kupitia bodi ya mikopo TCU.
“Kisheria wanapaswa kushirikisha serikali hadi kufikia hatua ya kupandisha gharama hizi, maana huyu ndio baba na mlezi wetu, sio mtu anakurupuka na kubandika tangazo gharama zimepanda kutoka kiasi hiki hadi kufikia hapa…hivi tunavyoongea kuna madaktari wataanza kufukuzwa leo eti hawajalipa,” alisema mmoja wa wanachuo.
St. Francis ni chuo kikuu kishiriki cha chuo kikuu cha St. Augustine (SAUT), kilichopo jijini Mwanza, ambacho mbali na kuzalisha madaktari kinajishugulisha na tafiti mbalimbali za magonjwa ukiwemo wa malaria hivyo kukifanya kuwa bora na kimbilio la wasomi katika fani ya udaktari nchini.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa