Home » » Kibadeni aing’arisha Mahakama Shimiwi

Kibadeni aing’arisha Mahakama Shimiwi


Scan10178
Wachezaji wanawake wa mchezo wa kamba wa timu ya Mahakama walishindana na wapinzani wao wa Mipango kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro katika mashindano ya Shimiwi inayoendelea mpaka sasa. Mahakama ilishinda kwa 2-0. (Picha/Mpigapicha wetu).
Na Mwandishi wetu, Morogoro
Timu ya  Mahakama ya Tanzania imeendeleza wimbi la ushindi katika michezo ya Shirikisho ya  Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (Shimiwi) inayoendelea mkoani Morogoro kwenye uwanja wa Jamhuri.
Timu ya Mahakama ambayo inanolewa na kocha wa zamani wa klabu ya Simba na timu ya Taifa, Abdallah “King Mputa” Kibadeni jana iliibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Ras Tanga na kuingia hatua ya robo fainali.
Wakati timu ya soka ikiingia katika hatua hiyo muhimu, timu ya mchezo, kamba (wanawake na wanaume) na netiboli nazo zimeingia katika hatua hiyo ya mtoano itakayoanza kesho kwenye uwanja wa huo.
Kamba wanaume watacheza na Waziri Mkuu wakati wanawake watapambana na Uchukuzi wakati netiboli itaonyeshana kazi na Uchukuzi pia. Katika mchezo wa jana wa soka, mabao ya Mahakama yalifungwa na Kinei Mwanzini, Michael Turuka, Jackson Ndaweka, Christopher David na Mike Cassian.
Awali, timu hiyo ilishinda dhidi ya Mipango kwa bao 1-0 kabla ya kuisambaratisha Maliasili kwa mabao 2-0 na baadaye kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Uchukuzi.
Scan10179
Timu ya Mahakama kwenye picha ya pamoja na kocha wa zamani wa klabu ya Simba na timu ya Taifa, Abdallah “King Mputa” Kibadeni (waliosimama kulia).
Kiongozi wa timu hiyo, Twaha Ali alisema kuwa wamefarijika na mwenendo mzuri wa timu zao na matumaini yao kuibuka washindi kwa michezo yote. “Tupo vizuri katika kila mchezo, tunatarajia kufanya vyema na kutwaa ubingwa mwaka huu,” alisema Ali.
Mratibu wa timu hiyo,Mushumbuzi Samweli alisema kuwa mashindano hayo ni magumu kutokana na maandalizi ya kila timu, hata hivyo watafanikiwa kurejea na ushindi.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa