Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa ugonjwa wa fistula, wameanza kutoa matibabu ya ugonjwa huo ambako tayari wagonjwa 20 wamelazwa kwa ajili ya kutibiwa.
Wagonjwa hao 20 kati yao tisa wameshafanyiwa upasuaji katika kambi maalum iliyoanza Oktoba 13 hadi 24 mwaka huu hospitalini hapo na wamelazwa kwa uangalizi zaidi.
Akizungumza katika uzinduzi wa matibabu ya Fistula uliofanyika katika hospitali hiyo, Mtaalamu wa upasuaji, Dk. John Ndumbaro, alisema bado wanakabiliwa na changamoto ya vitendea kazi ikiwemo kuwa na kitanda kimoja tu kwa ajili ya utoaji wa huduma hiyo na uhaba wa wataalam.
Aidha, Dk. Ndumbaro, ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya fistula, aliwahimiza mabinti kuepuka mimba za utotoni ambazo ni miongoni mwa visababishi vya ugonjwa huo sambamba na wajawazito kuhudhuria kliniki kwa wakati.
Kambi hiyo maalum ikimalizika, zoezi endelevu la matibabu kwa wagonjwa wa fistula litaendelea kufanywa bure kwa ufadhili wa shirika la Amref Health Africa katika hospitali hiyo, ambayo tangu mwaka 2009 walipoanza kutoa huduma isivyo rasmi, hadi sasa wameweza kuwafanyia tiba wagonjwa 176 wa fistula na kupona kabisa.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro katika uzinduzi wa kambi hiyo, Kaimu Mganga Mkuu Mkoa, Dk. Samson Tarimo, aliwahakikishia wananchi kuwa fistula inatibika na inaweza kuepukika, hivyo kina mama wanaopatwa tatizo hilo wasijifiche majumbani bali wafike kwenye vituo vya afya vilivyo jirani kwa ushauri wa kitaalamu.
chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment