Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JAMII imetakiwa kuacha imani potofu na kutoa ushirikiano kikamilifu
katika ukusanyaji wa takwimu kwa kila kaya nchini ili kuwezesha
Serikali kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo katika kuboresha
huduma na sera ili kuwa na maamuzi yanayotekelezeka.
Rai hiyo, imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, (Sera),
Mwigulu Nchemba, mwishoni mwa wiki wakati akifungua mafunzo ya
wasimamizi na wadadisi wa kufuatilia hali ya umaskini katika kila kaya
Tanzania, yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Nchemba, alisema imani potofu na za kizamani za jamii, zinaweza
kufanya shughuli za maendeleo kurudi nyuma ikiwemo kupanga mipango
muhimu.
Alisema kuwa, ikiwa wataendekeza imani hizo na kushindwa kutoa taarifa
sahihi za kitakwimu, watasababisha mipango ya maendeleo ikiwemo ujenzi
wa shule, zahanati na masoko kutojengwa kulingana na idadi ya watu
katika maeneo yao na kuwafanya kuanza kuhoji kulikoni.
Aidha, alisema wizara hiyo itaendelea na juhudi ya kuiwezesha kifedha
Ofisi ya NBS, ili iweze kuendelea na jukumu lake la kufikisha matokeo
ya tafiti zinazofanyika katika ngazi zote za utawala.
Akielezea kuhusu Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa
mwaka 2011/2012, alisema umaskini wa chakula umepungua kutoka asilimia
11.8 mwaka 2007 na kufikia asilimia 9.7 mwaka 2011/2012 wakati ule wa
kipato umetoka asilimia 34.4 mwaka 2007 na kufikia asilimia 28.2
2011/2012.
Alibainisha kuwa, matokeo hayo ni jambo la kujivunia kuona kwamba,
juhudi za Serikali zimefanikisha kufikia lengo la kupunguza umaskini
uliokithiri, yaani umaskini wa chakula kama ilivyoainishwa kwenye
Mkukuta I na II.
Hata hivyo, alisema lengo la kupunguza umaskini wa chakula lilikuwa
kufikia asilimia 12.9 ifikapo 2015 na matokeo yanaonyesha kuwa, Serikali
imevuka lengo hilo miaka mitatu kabla kwa kufikia asilimia 9.7.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, alisema wasimamizi na
wadadisi 65 wa ofisi hiyo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na
Zanzibar, wanapatiwa mafunzo ya wiki tatu kuhusu namna ya kukusanya
takwimu zinazohusiana na utafiti wa kufuatilia hali ya umaskini katika
Kaya Tanzania.
Alisema mafunzo hayo ni ya awamu ya nne na wale watakaofaulu
watashiriki katika zoezi hilo ambalo linategemewa kuanza Oktoba mosi
mwaka huu na kuendelea kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Hata hivyo, alisema madososo ya utafiti huo, pia utakusanya taarifa za
sekta nyingine muhimu ambazo zinaweza kuchambuliwa kwa kuhusishwa na
hali ya umaskini.
Dk. Chuwa, alizitaja sekta hizo kuwa ni kilimo, uvuvi, mifugo, afya, ajira na upatikanaji wa huduma mbalimbali katika kaya.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment