Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Tangu Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na timu yake waanze
ziara ya kikazi katika baadhi ya mikoa wiki iliyopita, wamesikika
wakitoa kauli katika mikutano ya hadhara ambazo zimechukuliwa na baadhi
ya wananchi kwamba zinaidhoofisha Serikali ya chama hicho. Wengi
wamediriki kusema kwamba hali hiyo imejenga picha kwamba kauli za
viongozi hao zinaonyesha kuwapo mvutano kati ya viongozi wa Serikali na
chama hicho tawala, kwani hali kama hiyo imekuwa ikijitokeza pindi
sekretarieti ya chama hicho inapofanya ziara katika sehemu mbalimbali
nchini na kuhutubia mikutano ya hadhara.
Itakumbukwa kuwa, sekretarieti hiyo ilipofanya
ziara ndefu mikoani miezi kadhaa iliyopita, tulishuhudia mikutano yake
ya hadhara ikielekeza mashambulizi dhidi ya mawaziri wa Serikali. Pamoja
na kuwaita baadhi ya mawaziri ‘mizigo’ na kumtaka Rais Jakaya Kikwete
awafukuze kazi kwa kile viongozi hao walichokiita utendaji mbovu katika
kutatua kero za wananchi, tulishangaa kuona tuhuma hizo dhidi ya
mawaziri hao zikitolewa hadharani kwa mtindo ulioonekana kuwadhalilisha.
Baadhi ya mawaziri walilalamikia kitendo hicho na huenda Rais Kikwete
alisikiliza kilio chao kwa kuwa waliendelea na nafasi zao za uwaziri.
Ni katika muktadha huo, baadhi ya wananchi
wanasema hotuba nyingi zinazotolewa sasa na viongozi wa sekretarieti
hiyo walio katika ziara ya mikoa mbalimbali, ikiwamo Pwani na Tanga
zinaichonganisha Serikali na wananchi. Maudhui ya hotuba nyingi
wanazotoa hayalengi kuwaeleza na kuwaelimisha wananchi kuhusu hatua
zinazochukuliwa na Serikali ya chama hicho katika kutatua matatizo yao,
bali hotuba hizo zimetawaliwa na lawama, malalamiko na hasira dhidi ya
Serikali ambayo imeundwa na chama chenyewe. Katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Chalinze, mkoani Pwani juzi, kwa mfano, katibu mkuu huyo wa
CCM alihoji utaratibu aliouita mbovu wa matumizi ya mashine za
kielektroniki za kutunza hesabu za wafanyabiashara (EFD), akisema bei ya
mashine hizo ni kubwa na kuna upungufu katika sheria inayohusu matumizi
ya mashine hizo.
Huku akisema baadhi ya malalamiko ya
wafanyabiashara ni ya msingi na yanapaswa kushughulikiwa, alisema
wanaopinga matumizi hayo wako sahihi kabisa, huku akisisitiza kwamba
kuna upungufu katika sheria inayohusu matumizi ya mashine hizo, hivyo
wafanyabiashara wanaopinga matumizi yake wasionekane kama wakorofi.
Alisema watu wanapopinga matumizi ya mashine hizo wanaambiwa wanavunja
sheria wakati sheria yenyewe imepinda. Hata hivyo, swali la kujiuliza ni
kwa nini chama hicho hakikuchukua hatua ya kuondoa udhaifu huo?
Sisi hatuna ugomvi na kauli hiyo kama ambavyo
tumekuwa hatuna ugomvi na kauli zake nyingine ambazo yeye na timu yake
wamekuwa wakizitoa katika mikutano ya hadhara. Ugomvi pekee tulionao ni
kauli hizo kutolewa katika mikutano ya hadhara ambayo inaweza
kusababisha baadhi ya wafanyabiashara kugoma kutumia mashine hizo kwa
kauli hizo. Moja ya majukumu ya chama tawala popote duniani ni kutunga
na kusimamia sera mbalimbali na kuhakikisha Serikali inazitekeleza. Pale
inaposhindwa kufanya hivyo, chama tawala huchukua hatua stahiki, siyo
kupitia katika mikutano ya hadhara ambapo watu hutaka kuambiwa tu yale
wanayotaka kusikia.
Sisi tunaamini kuwa kila mfanyabiashara anapaswa
kulipa kodi na tungependa suala la EFD lisichukuliwe kisiasa, ila
wataalamu waachwe wafanye kazi yao bila kuingiliwa na wanasiasa.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment