Home » » DIWANI AWAPA TUZO WADAU WA MAENDELEO

DIWANI AWAPA TUZO WADAU WA MAENDELEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
DIWANI wa Mngeta Felisian Kigawa (CHADEMA) amempa Tuzo ya uongozi uliotukuka Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Hassan Masala kwa usimamizi bora ulioharakisha maendeleo ya kata.
Pamoja na Masala, wengine waliopata tuzo na vyeti ni Padri Egfrid Tonz waliochangia maendeleo ya tarafa ya Mngeta, kampuni ya KP, Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo na Camfed.
Tuzo hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya uzinduzi wa vyumba viwili vya maabara kwenye shule ya sekondari Kiburubutu vilivyojengwa kwa hisani ya DEZA na serikali ya Uswiss likiwa ni ombi la Padri Tonz wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mchombe wilayani humo.
Kwa mujibu wa diwani Kigawa wazo la tuzo kwa mkuu huyo wa wilaya linatokana na ombi la wanachi kumpendekeza apate tuzo hiyo kwa kuwa anathamini mchango wake kwa wanachi hasa anavyotumia muda wake kushughulikia kero za wananchi.
“Mpaka sasa padri huyu amejenga ushawishi kwa wahisani na rafiki zake nje ya nchi wakiwemo DEZA na Novatis wa Uswiss ambao wametumia zaidi ya sh milioni 586 kwa ajili ya miradi ya kijamii,” alifafanua diwani huyo.
Aliitaja miradi iliyowezeshwa na padre huyo kuwa ni ujenzi wa bweni la wavulana na kisima cha maji Nakaguru sekondari, jengo la utawala, maabara mbili na kisima cha maji shule ya sekondari Kiburubutu.
Miradi mingine ni nyumba mbili za walimu, tanki la maji, bweni la wasichana na maabara moja katika shule ya sekondari Mchombe.
Alisema KPL kupitia ruzuku za vijiji ilijenga vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Ilole, vyumba vitatu vya madarasa na ofisi ya shule ya msingi Luvirikila, utengenezaji wa samani za shule za Mkangawalo na Itongowa, ujenzi wa chumba kimoja cha darasa sekondari ya Mchombe na kuboresha mtandao wa maji vijiji vya Mkangawalo na Mngeta.
Kuhusu tuzo ya mkurugezi na shirika la Camfed alisema amepewa kutokana na uwezo wake wa kutekeleza miradi kwa kipindi kifupi na kugharimia mahitaji muhimu ya wanafunzi wa kike na yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Katika shukarani zao Padre Tonz raia wa Uswiss mwenye miaka 88 aliyeingia nchini mwaka 1955 alisema anafarijika kuona baadhi ya malengo yake yanatimia licha ya changamoto za kibinadamu anazokutana nazo.
Kwa upande wake kuu wa wilaya ya Kilombero Masala alimpongeza diwani huyo kwa ubunifu na kuwataka viongozi wa serikali wilayani humo kuwa wabunifu kwa kutafuta njia rahisi ya kuhamasisha wanachi hususani vijana kushiriki katika uzalishaji zaidi ya kubaki tegemezi
 Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa