Home » » JK:NITAWAWAJIBISHA VIONGOZI WANAOCHOCHEA MIGOGORO YA ARDHI

JK:NITAWAWAJIBISHA VIONGOZI WANAOCHOCHEA MIGOGORO YA ARDHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais Jakaya Kikwete
 
Rais Jakaya Kikwete amegeuka mbogo kwa kusema kuwa amechoshwa na migogoro ya ardhi na kuwatishia kuwawajibisha viongozi wa wilaya ya Kilosa na Mkoa wa Morogoro kwa kuwa baadhi yao  ndiyo chanzo cha mapigano kati ya  wakulima na wafugaji.
Amesema viongozi hao wamekuwa wakipokea hongo kutoka kwa wafugaji na kuruhusu kuingia kwa idadi kubwa ya mifugo kuliko maeneo ya malisho na kusababisha migogoro.

Amesema  sasa amechoka kusikia mapigano kati ya wakulima na wafugaji na kuwataka viongozi hao kubadilika mara moja vinginevyo atawawajibisha kwa kushindwa kusimamia amani katika maeneo yao.

Rais Kikwete alisema hayo mara baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kupitia kwa Wabunge wao Abdsalaam Sas (Mikumi) na Mustafa Mkullo (Kilosa) wakati wa ziara yake inayoendelea mkoani Morogoro  ya kukagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema kuwa viongozi hao wamekuwa chanzo hicho cha migogoro kwa sababu wanapokea ndama na madume ya ng’ombe kutoka kwa wafugaji wanaoingia kinyemela katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Kilosa wakiwa na idadi kubwa ya mifugo huku wakijua hakuna maeneo ya malisho.

“Nyinyi viongozi wa wilaya na mkoa mmekuwa mkigaiwa ndama na kupokea madume ya ng’ombe ndiyo mmekuwa chanzo cha kuzuka kwa mapigano ya wakulima na wafugaji  kwakuwa wanakuwa na jeuri ya kuingiza ng’ombe katika mashamba ya wakulima, hivyo acheni mara moja vinginevyo tutawawajibisha tu,” alisema Rais Kikwete.

Alisema kuwa suala la mapigano kati ya wakulima na wafugaji limekuwa likileta uhasama na  kuligharimu Taifa kutokana na mauaji, hivyo aliwezi kuachiwa hivi hivi, ni lazima lipatiwe ufumbuzi kupitia kwa viongozi hao kwa kusimamia sheria zilizopo ikiwamo ya kuwaeleza wafugaji wanaovamia kuwa ardhi ya eneo hilo haitoshi.

“Sasa viongozi wa vijiji mnapaswa kuwambia ukweli wafugaji wanaokuja katika maeneo yenu kuwa hapa pamejaa, mkiwaachia wakingia ndiyo wanaswaga mifugo katika mashamba ya wakulima matokeo yake ndiyo mapigano hilo hatutokubali kuona mauaji yanatokea,” alisema.

Alisema iwapo wafugaji wataazimia na kuacha kulisha mifugo yao katika mashamba ya mazao ya wakulima, kamwe hakutatokea migogoro baina yao na wakulima .

Alisema kimsingi jamii hizo zinategemeana , kwa mkulima kutegemea mfugaji katika  kupata nyama ‘kitoweo’ na mfugaji kumtengemea mkulima katika kupata chakula ugali ama wali kutokana na mazao yanayolimwa na wakulima.

Rais Kikwete alisema, kila anakopita mikoani amekuwa akipokea malalamiko juu ya wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima hali inayozua tafrani na migogoro isiyomalizika.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa