Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Jakaya Kikwete
“Nilishatoa maagizo kama miezi michache iliyopita kuwa kila mkuu wa wilaya ahakikishe anajenga maabara katika shule zake za kata sasa watu wanafikiri ni mchezo wataniona miezi miwili ijayo kama nilikuwa natania,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema hayo wakati akiongea na wananchi wa Manispaa ya Morogoro katika ziara yake inayoendelea wilaya zote kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuweka mawe ya msingi.
Alisema alitoa agizo kwa wakuu wa wilaya zote kujenga maabara hizo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu lakini mpaka sasa wapo baadhi yao hawajaanza ujenzi huo.
Alisema moja ya wakuu wa wilaya hao ni waliopo katika mkoa wa Morogoro ambao umepangiwa kujenga jumla ya maabara 69 lakini mpaka sasa wamejenga maabara 10 huku wakiwa wamebakisha miezi miwili.
“Tulikubaliana kujenga majengo ya maabara katika shule zote za kata, lakini hapa naona mko nyuma mlitakiwa kujenga maabara 69 mpaka sasa mmejenga 10 sasa tutaulizana Novemba na sitamuonea haya kumshughulikia mkuu yoyote wa wilaya,” alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu ukosefu wa maji katika manispaa ya Morogoro, Rais Kikwete alisema kunatokana na viongozi wa wilaya ya Morogoro kushindwa kuwaondoa watu wanaofanya uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji.
Aliwaagiza viongozi hao kuhakikisha wanawaondoa mara moja wale wote waliojenga katika vyanzo vya maji na kuacha kusikiliza viongozi wa kisiasa.
Kuhusu suala la afya, alipongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na uongozi huo kwa kuboresha huduma hizo ikiwemo kujenga hospitali ya wilaya na ujenzi wa wodi ya wajawazito hatua ambayo itapunguza vifo kwa akina mamawajawazito. Katika hatua nyingine Rais Kikwete amesema iwapo wafugaji wataazimia na kuacha kulisha mifugo yao katika mashamba ya mazao ya wakulima kamwe hakutatokea migogoro baina yao na wakulima .
Alisema kimsingi jamii hizo zinategemeana, kwa mkulima kutegemea mfugaji katika kupata nyama ‘kitoweo’ na mfugaji kumtengemea mkulima katika kupata chakula.
Kauli hiyo ya Rais aliitoa kwa nyakati tofauti mara baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wabunge wa majimbo ya Kilombero na Morogoro Kusini, kuwa wafugaji wamekuwa kero katika maeneo yao ambayo inahitaji ufumbuzi wa kudumu.
Rais Kikwete alisema, kila anakopita mikoani amekuwa akipokea malalamiko juu ya wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima hali inayozua tafrani na migogoro isiyomalizika.
Alisema , katika wilaya za mkoa wa Morogoro na maeneo mengine nchini jamii ya wafugaji imekuwa ikizua mapigano ambayo yameleta madhara makubwa miongoni mwao na chanzo ni wafugaji kuungiza mifugo yake kwenye mashamba ya wakulima.
Hata hivyo Rais Kikwete alisema, ili kumaliza migogoro hiyo sehamu mbalimbali nchini ni lazima wafugaji waache tabia ya kuchunga mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
Katika ziara ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Rais alizindua mradi wa maji kwa wananchi wa Duthumi na jengo la upasuaji katika kituo cha afya Duthumi, ufunguzi wa soko la matombo na kuzungumza na wananchi.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment