Home » » CHADEMA WAJA NA MAANDAMANO YA `MCHAKAMCHAKA WA KATIBA`

CHADEMA WAJA NA MAANDAMANO YA `MCHAKAMCHAKA WA KATIBA`

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Katibu wa Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) John Mnyika, akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani), Rasimu ya Katiba jijini Dar es Salaam jana.
 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho ni sehemu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kimesema kimeanza maandalizi ya maandamano kiliyoyaita “Mchakamchaka wa Katiba” yaliyoitishwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda Ukawa yanayotarajiwa kufanyika nchini kote kudai upatikanaji wa katiba mpya itakayoridhiwa na wananchi wote kutokana na vikao vya Bunge hilo kutositishwa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Chadema,  John Mnyika, aliwaambia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana kuwa maandalizi ya maandamano hayo yanaendelea licha ya mazungumzo aliyoyaita ya “nyuma ya pazia” baina Ukawa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kutafuta maridhiano yakiendelea.

Alisema wamelazimika kuendelea na maandalizi ya maandamano hayo kutokana na wenzao wa CCM, nao kuridhia vikao vya Bunge hilo kuendelea, huku mazungumzo hayo yakiendelea.

“Kama wanataka tusitishe maandamano, na wao wasitishe Bunge,” alisema Mnyika.

Hata hivyo, Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema kuendelea kwa mazungumzo hayo ni jambo la heri, ingawa tija yake ni ya matumaini ya mashaka.

“Tunaamini (mazungumzo) yanaweza kuleta miujiza,” alisema Mnyika.Aliwataka wana Chadema nchini kote kuendelea na maandalizi ya maandamano hayo.

Alisema kwa upande wa idara ya mawasiliano na uhusiano ya chama anayoiongoza, wameandaa wimbo maalumu uitwao: “Mchakamchaka wa katiba”, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maandamano hayo.

Mnyika alisema Kamati Kuu (CC) ya CCM kushindwa kuagiza vikao vya Bunge hilo visitishwe ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, imekosea.

Alisema pia imekosea kumwagiza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kukutana na Ukawa kutafuta maridhiano, kwa kuwa hajachaguliwa na wananchi, badala yake, ilipaswa imwagize Rais Kikwete atumie madaraka yake kuingilia kati kunusuru mchakato wa katiba mpya kwa kuwa yeye ndiye aliyechaguliwa na wananchi.

Alisema kitendo cha CC kushindwa kufanya hivyo, kimethibitisha kauli ya onyo iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere enzi za uhai wake dhidi ya CCM kwamba, “chama legelege huzaa serikali legelege” na kwamba, Rais Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wake, ameshindwa kuondoa udhaifu huo wakati CC ilipojadili ajenda ya mchakato wa katiba mpya.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa