Home » » WAKULIMA 300 WA KILOSA, CHAMWINO KUPIGWA JEKI

WAKULIMA 300 WA KILOSA, CHAMWINO KUPIGWA JEKI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399

SERIKALI ina mpango wa kufikia wakulima 300 wa wilaya za Kilosa mkoani Morogoro na Chamwino mkoani Dodoma. Lengo la mpango huo ni kusaidia kutambua changamoto za kilimo zinazowakabili na namna ya kuzipatia suluhu.
Mpango huo ni utekelezaji wa mradi wa kuelimisha wakulima ujulikanao kama Trans Sec, wenye kuhakikisha usalama wa chakula nchini na kuongeza thamani ya mazao ili kuleta mabadiliko katika kilimo.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mratibu wa Mradi huo, Profesa Siza Tumbo wakati akizungumza katika warsha iliyokutanisha wadau na wataalamu kujadili kuhusu utekelezaji wa mradi huo.
“Huu mradi unafanyika Tanzania pekee… na kila wilaya hizo utawafikia wakulima hao 150, utakuwa ni mradi shirikishi ukianzia ngazi ya chini hadi ya taifa,” alisema Profesa Siza.
Alisema mradi huo unafanyika katika wilaya hizo kama mfano na baadae utaenezwa nchi nzima na utawashirikisha wananchi kwa kujua matatizo yanayowakabili, ikiwemo masoko na kupanga namna ya kuyapatia ufumbuzi.
Alisema katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, mkazo wa uzalishaji utakuwa kwenye mazao ya mtama, alizeti na karanga, ambayo yalikuwa yakiachwa bila kupatiwa kipaumbele, jambo ambalo limekuwa likimuacha mkulima katika hali yake ya asili bila kuona mabadiliko ya kilimo.
Akizungumza katika warsha hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu, wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Sophia Kaduma, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, David Biswelo alisema mradi huo unatekelezwa kwa wakati muafaka ili kuimarisha usalama wa chakula kuanzia ngazi ya vijiji.

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa