Waziri
Mkuu, MIzengo Pinda , Viongozi wa Baraza la Mazingiea nchini, NEMC na
viongozi wa mkoa wa Morogoro wakitazama maji yenye sumu, kemikali na
tindikali yaliyoekekezwa mtoni yakitoka kwenye viwanda vya 21st Century
cha nguo, Morogoro Canvanse na kiwanda cha magunia cha Morogoro wakati
alipotembela eneo Kihonda mbuyuni kukagua athari za maji hayo.(Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………. .
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda ametoa mwezi mmoja kwa Baraza la Taifa la Mazingira
(NEMC) iwe imetoa mapendekezo kwa Serikali kuhusu matumizi ya maji
machafu yanayotokea kwenye viwanda vinne vya ngozi, magunia, nguo na
maturubali (canvas).
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumamosi, Desemba 7, 2013) mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye kiwanda cha nguo cha 21st Century kilichopo eneo la Kihonda Viwandani nje kidogo ya mji wa Morogoro.
Akizungumza
na uongozi wa mkoa, wilaya, kiwanda hicho pamoja na NEMC ya mara baada
ya kutembelea eneo ambalo limeathirika na maji yanayotiririka kutoka
kwenye viwanda hivyo, Waziri Mkuu alisema tatizo lililopo linachangiwa
na kutokuwepo kwa mtu au taasisi maalum ya kusimamia mabwawa ya mfumo wa
majitaka (waste management ponds).
“Viwanda
hivi vilibinafsishwa lakini mfumo wa usafishaji majitaka
haukubinafsishwa… NEMC iishauri Serikali nini kinapaswa kifanyike.
Ifanye utafiti kuhusu matumizi ya majitaka yanayotoka kwenye viwanda
hivi na ilete uchambuzi huo Serikalini,” alisema.
Waziri
Mkuu ambaye alitembelea eneo la Kihonda Mbuyuni katika kata ya Mafisi
ambako maji hayo yanaingia korongoni na kuelekea mto Ngerengere,
alishuhudia mifereja ya maji machafu yenye harufu kali na rangi
mchanganyiko ya kijani na bluu ikitiririka katikati ya nyumba za watu.
“Hatuwezi
kuendelea na hali hii ya kutiririsha maji kwenye makazi ya watu, ni
bomu litakalolipuka hivi karibuni. Kuna watoto wanacheza katika maeneo
yale wanaweza kunywa au kunawa yale maji, kuna mifugo inapita, inaweza
kunywa yale maji, ni hatari kwa kila mmoja wetu,” alisisitiza.
Aliitaka
NEMC iangalie uwezekano wa kumpatia mtu binafsi aendeshe mfumo huo hata
kama itabidi asimamiwe na Halmashauri lakini kinachotakiwa ni
kupatikana kwa mtu mwenye uwezo wa kuendesha mfumo huo kwa utaalamu.
Aliipa
NEMC miezi miwili ili iwe imekamilisha utafiti wake pamoja na kuangalia
uwezekano wa kumpata mtaalamu wa kuifanya kazi hiyo.
Alitoa
pia mwezi mmoja kwa Manispaa ya Morogoro kuwa imetafuta eneo jipya na
kubwa zaidi kwa ajili ya kumwaga takataka kwani dampo lililopo katika
kata hiyo linachangia uchafuzi wa mazingira na kuleta kero kwa wananchi.
“Wakati
ule dampo linaletwa huku ilikuwa ni sahihi kwa sababu huku kulikuwa ni
nje ya mji lakini kwa sasa siyo sahihi. Nimemwambia Meya akae na watu
wake wafikirie kujenga dampo jingine la kisasa… watafute eneo kubwa na
kuwe na mifumo ya kisasa,” alisema.
Kuhusu
matumizi ya kuni katika kiwanda hicho, Waziri Mkuu alisema hakubaliani
kabisa na matumizi ya kuni kwa sababu yanachangia uharibifu mkubwa wa
mazingira. Aliutaka uongozi wa kiwanda hicho, uendelee na mpango wake
mpya wa kutumia makaa ya mawe au hata kuangalia mpango wa kutumia umeme
utakaotokana na gesi.
“Najua
kuna gharama katika kubadilisha mfumo wa boilers zenu lakini matumizi
ya tani 50 za magogo kwa siku hapana! Tani 50 nazilinganisha na magunia
500 ya mahindi, sasa kwa miezi sita au kwa mwaka mmoja, mtatumia kuni
kiasi gani? Si Morogoro nzima itateketea? Alihoji Waziri Mkuu.
Akijitetea
kuhusu suala hilo, mmiliki wa kiwanda hicho, Bw. Gulam Dewji alisema
moto unaotokana na makaa ya mawe hauna nguvu ya kutosha kuzalisha mvuke
wa kuzalisha umeme wa kuendeshea mitambo ya kiwanda hicho. “Tumeomba kwa
mwaka mmoja tu tupewe ruhusa ya kuchanganya makaa ya mawe na vipande
vya miti hadi tutakapopata boilers mpya,” alisema.
Waziri
Mkuu alimweleza Bw. Dewji asubiri majibu ya maombi yake kutoka NEMC
ambako maombi hayo yalipelekwa lakini pia akawaonya viongozi wa NEMC
kuwa makini wakati wanapitia maombi hayo ili waweze kuwa na mbinu za
kubainisha kama kweli vitatumika vipande vya miti au watarudia utaratibu
wao wa zamani wa kutumia magogo lakini wanayakata katika vipande vidogo
vidogo.
Hata
hivyo, katika kikao hicho Meya wa Manispaa ya Morogoro, Bw. Amiri Nondo
na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bw. Said Amanzi walielezea kutoridhishwa
kwao na uhusiano uliopo baina ya uongozi wa kiwanda hicho na mamlaka
zilizopo wakidai kufungiwa mageti na kutotekelezwa kwa maelekezo
yanayotolewa na mamlaka husika.
Waziri
Mkuu alimtaka mmiliki wa kiwanda hicho, Bw. Gulam Dewji ajenge
mahusiano mazuri na uongozi wa mkoa kwa sababu viwanda vyake viko katika
mkoa huo na hivyo hana budi kuzingatia maslahi ya wakazi wa Morogoro
kwanza. “Wao ni viongozi wa mkoa lakini pia ni wawakilishi wa wananchi,
kwa hiyo wanawajibika kwa wananchi, linapotokea jambo wao ndiyo
wataulizwa na wananchi,” alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment