Na Hamida Shariff, Morogoro.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Tamisemi Hawa Ghasia amesema kuwa Serikali inakiri kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa fedha katika chaguzi mbalimbali hivyo imekuwa ikiongeza kiwango cha fedha katika kugharamia chaguzi hizo.
Hayo aliyasema jana mjini hapa wakati akifungua mkutano wa viongozi wa asasi za kiraia nchini wa kujadili maoni ya kuboresha kanuni za uchaguzi wa viongozi wa Mamlaka za serikali za mitaa kwa ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa.
Waziri Ghasia alisema kuwa kwa mwaka 2009 Serikali iligharamia ununuzi wa masanduku ya uchaguzi, karatasi za kupigia kura na pia gharama za kuhakikisha vifaa hivyo vinafika mahali panapostahili ambapo gharama zote hizo zilikuwa takribani Sh. 3 bilioni.
Alisema kuwa kwa mwaka 2014 Serikali imetenga Sh 15 bilioni kwa ajili ya shughuli za uchaguzi huo na kwamba fedha hizo zitafanyakazi ya kuandaa karatasi za kupiga kura, ununuzi wa nyongeza ya masanduku ya kupigia kura, kuendesha semina za uchaguzi, ununuzi wa vipeperushi na fedha nyingine zitapelekwa Halmashauri na kwenye Sekretarieti za mikoa kwa ajili ya kugharamia shughuli za uchaguzi.
Aidha alisema kuwa bajeti ya uchaguzi wa mwaka 2009 ikilinganishwa na bajeti iliyotengwa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu kuna ongezeko la jumla ya Sh.12 bilioni hivyo ni matarajio ya serikali kwamba bajeti hiyo itakidhi mahitaji ya shughuli za uchaguzi huu wa viongozi wa Serikali za mitaa katika maeneo yaliyokusudiwa.
Hata hivyo alisema kuwa serikali ipo tayari kupokea mawazo na ushauri utakaotolewa na asasi za kiraia ili kuendesha uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2014 kwa mafanikio na hiyo ni pamoja na kuendesha uchaguzi katika misingi ya uwazi, usawa, na haki na hivyo kuweka uwanja mpana kwa vyama vyote vya siasa na kwa wananchi kushiriki katika uchaguzi huo.
Naye Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Tamisemi Aggrey Mwanri alisema kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi kama Tamisemi wanafanya maandalizi mbalimbali ya kuhakikisha changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizopita hazijirudii katika uchaguzi huu.
Waziri Mwanri alisema kuwa maandalizi hayo ni pamoja kukusanya maoni na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali kupitia mikutano na kwa kuanza wameamua kushirikisha mashirika na asasi za kiraia kwani ndio kiungo cha wananchi na yatawasaidia kupata changamoto, maoni na ushauri ambao utafanyiwa kazi ili kuboresha uchaguzi huo. Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment