Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
VIONGOZI wa serikali za vijiji vya Kata ya Maguha na Magubike,
mkoani Morogoro, wameazimia kusambaratisha na kukomesha migogoro ya
ardhi kwa kuvifikisha mahakamani vikaratasi vyote vya kugawana ardhi
kwa njia ya panya.
Maazimio hayo yaliyofikiwa mwishoni mwa wiki kwenye mafunzo ya sera
na sheria za ardhi nchini yaliyoandaliwa na asasi ya Dira na Foundation
for Civil Society – FCS, yalikwenda sambamba na mchakato wa kutunga
sheria ndogondogo katika vijiji hivyo kuwadhibiti viongozi
watakaokiuka.
Sambamba na maazimio hayo, pia wamekubaliana hadi kufikia Agosti
mwaka huu, vijiji viainishe na kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi
katika vijiji husika, viwe na masijala na wananchi wapatiwe hati za
kimila kumiliki ardhi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao wakiongozwa na Diwani
wa Magubike, Ernest Chilolo na Mtendaji Kata, James Mnghondwa, walisema
wamechoshwa na migogoro isiyoisha na kurudisha nyuma maendeleo ya
wananchi.
“Cha msingi hakuna haja kukaa tukiwalea wanaotuangamiza, ni bora
tukaonekana wabaya kwa kuzuia ardhi yetu isiporwe na wachache kwa faida
zao na kutuacha tukiumia,” alisema Diwani Chilolo.
Akihitimisha mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Dira, Erasmo Tulo,
alisema tayari asasi hiyo imeendesha mafunzo kwa sanaa vijijini humo na
kubaini changamoto mbalimbali ikiwemo ya wananchi kutozielewa sera na
sheria za ardhi na kusababisha migogoro isiyoisha.
“Hii ni awamu ya pili ya mafunzo haya, tunachotegemea kwenu kwanza ni
migogoro ipungue kwa zaidi ya asilimia 90 na wananchi watendeeni haki
kwa kuwamilikisha ardhi, ili kila mmoja awe na nguvu ya umiki,”
alisema.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment