Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HALMASHAURI ya Morogoro, imetakiwa kuondoa dampo la taka
lililojengwa katika eneo la Mafisa, kabla ya Desemba mwaka huu, kwani
ni eneo la makazi ya watu.
Akizungumza katika ziara ya kushitukiza mbunge wa Morogoro Mjini,
AbdulAziz Abood, alisema kutokana na kukua kwa mji dampo hilo kwa sasa
linapaswa kuhamishwa kwa kuwa lipo jirani na makazi ya watu.
Abood alisema halmashauri hiyo ina eneo lingine lililopo nje ya mji
katika kata ya Mkundi lililotengwa kwa ajili ya kutupa taka.
Alisema hatua ya kuwepo kwa dampo hilo katika makazi ya watu inaweza
kuchangia kuwepo kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo kuharisha damu na
kipindupindu.
“Nimesikia kilio cha wakazi hao ambacho ni cha muda mrefu na diwani
wao amejaribu kila njia kutafuta muafaka wa suala hilo lakini bado
kuna kigugumizi cha kuondoa dampo hilo,” alisema.
Alisema halmashauri hiyo ina uwezo wa kuhamisha dampo hilo kwa kuwa
ina vitendea kazi vya kisasa yakiwemo magari ya kubeba taka.
Mbunge huyo alisema kuwa halmashauri haipaswi kuhofu gharama za
kuhamisha dampo hilo kwa kuwa hatua ya kuendelea kumwaga taka katika
eneo hilo ni sawa na kuweka rehani afya za wakazi hao.
Awali, wananchi wa eneo hilo walilalamikia hatua ya kuwepo kwa dampo
hilo katika makazi yao kwani, limekuwa likichangia kuwepo kwa harufu
mbaya ya uozo na nzi, huku pia wakilalamikia maji taka yanayomwagwa
kutoka viwandani ambayo yanahatarisha usalama wa afya zao.
chanzo :Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment