Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MFUKO wa Ufadhili wa Ukimwi (RFE), umetumia kiasi cha sh bilioni 36
kusaidia watoto yatima, wanaoishi na virusi na watu wanaotumia miili
yao kibiashara.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa mfuko huo, Profesa Saleh
Muhammed, alieleza hayo juzi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kupitia
utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na mfuko huo.
Alisema kiasi hicho cha fedha zaidi ya sh bilioni 36 kimetumika
katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi 215
kupatiwa ufadhili kwa lengo la kusaidia jamii.
Kwa mujibu wa Profesa Muhammed, taasisi hizo ni pamoja na
zinazojishughulisha na kuwajali na kuwasaidia watoto yatima na
wanaoishi kwenye mazingira magumu, watu walio katika hatari zaidi ya
kuambukizwa VVU kutokana na mazingira ya shughuli na tabia zao.
Aliyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na wanaotumia miili yao
kibiashara maarufu kwa jina la dada poa, wanaume wanaojamiiana na
wenzao, madereva wa masafa marefu na watu wanaojidunga sindano zenye
dawa za kulevya.
Alisema kutokana na taarifa ya Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi
(TACAIDS) na ile ya Zanzibar (ZAC) za hivi karibuni, kiwango cha
maambukizi mapya ya VVU kinatofautiana kutoka mkoa mmoja hadi mwingine
na yameripotiwa kupungua katika baadhi ya mikoa.
“Hali hii imetokana na kazi kubwa inayofanywa na serikali kuu,
halmashauri zetu na asasi zisizo za serikali kwa ushirikiano wa karibu
na asasi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na nchi zenye ubalozi hapa nchini
na Umoja wa Mataifa,” alisema.
Alisema tathmini iliyofanywa kwa pamoja na TACAIDS na ZAC kwa
ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Mwaka 2009 kuhusu utendaji
kazi na ufanikishaji wa shughuli za RFE, imeonyesha mfuko huo una
umuhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Meneja Mradi wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Mara, Rhobi Samwel,
alisema RFE imewawezesha kiasi cha sh milioni 198 walizozitumia
kuelimisha jamii.
Alisema Serengeti kuna tatizo la ukeketaji ambao wazazi wanalazimisha
watoto hadi leo kuwafanyia ukatili huo, hivyo wamekuwa wakitoa elimu
kwa wazazi kuwataka waache.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment