Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT),
Abraham Shamumoyo, amewataka madiwani kusimamia fedha za miradi ya
maendeleo zinazopelekwa na serikali kwenye halmashauri zao.
Shamumoyo alisema hayo jana wakati akikagua miradi ya maendeleo
kwenye maadhimisho ya Wiki ya Serikali za Mitaa mkoani hapa,
inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
Alisema kuna baadhi ya halmashauri zimeshindwa kusimamia miradi ya
maendeleo kwa ufanisi badala yake zimekuwa zikitumia fedha nyingi
kwenye miradi ambayo hailingani na thamani halisi ya fedha
zilizotumika.
“Kuna baadhi za halmashauri humu nchini ukienda unakuta miradi
iliyotekelezwa ipo chini ya viwango, hadi ukuta unataka kuanguka
kutokana na kujengwa chini ya kiwango,” alisema Shamumoyo.
Pia alishauri halmashauri kutekeleza miradi yake kwa ubora ili
kuongeza fedha pindi wanapotaka kuomba fedha za kuendesha miradi
mingine.
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Gulamhafeez Mukadam,
alisema tatizo la makandarasi wengi kujenga miradi chini ya viwango
limekuwa likisumbua halmashauri nyingi nchini.
“Kwa mfano kwetu Shinyanga, mradi mmoja umekuwa ukitekelezwa na zaidi
ya wakandarasi watatu hadi wanne kutokana na kila ukikagua unakutana
na upungufu, hali hii inachelewesha miradi mingi kukamilika kwa
wakati,” alisema Meya Mukadam.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Amir Kiroboto, alisema
siri ya mafaniko ya miradi yao kuwa bora inatokana na usimamizi mzuri
kuanzia kwa madiwani hadi kwa wataalamu wa halmashauri hiyo.
Chanzo:Tanznia Daima
0 comments:
Post a Comment