Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Maji,Profesa Jumanne Maghembe.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji ya Ziwa Victoria kutoka katika kijiji cha Mhalo hadi mji wa Ngudu wilayani Kwimba, Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe, alisema ni lazima wananchi kutunza vyanzo vya maji ili kuepuka ukame unaoweza kutokea kutokana na uharibifu huo wa mazingira.
Alisema serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa ili kuepuka matatizo ya kukumbwa na ukame usiokuwa wa lazima katika miji mingi hapa nchini.
“Tungependa wananchi wafahamu kuwa kutunza vyanzo vya maji ni kwa faida yao wenyewe, kwa vizazi vya sasa na vijavyo…kwa kufanya hivyo watajiwekea mazingira mazuri ya kujenga uchumi wa nchi,” alisema.
Aliongeza: “Rasilimali za maji zinapungua kwa kasi, hii yote ni kutokana na uharibifu wa mazingira,” alisema huku akitoa mifano ya maeneo kati ya mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Alifafanua kuwa wakati wa kiangazi maji yanakauka kabisa katika baadhi ya mito hapa nchini, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya binadamu na maisha ya viumbe waishio majini na nchi kavu.
“Ukipanda kwenye milima ya Usambara toka Korogwe hadi Bwiko utaona mito yote imekauka, mto pekee uliobaki ni ule wa Mkomazi, hii ni hatari,” alisema.
Aidha, Waziri Maghembe alielezea kuwa tatizo la mabadiliko ya tabianchi husababisha upungufu wa maji katika maeneo mengi na kuwa maeneo yaliyokuwa yanapata milimita 1,000 kwa mwaka sasa hivi yanapata milimita 500 kwa mwaka.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment