Home » » SUA yaanzisha kampeni kulinda Bwawa la Mindu

SUA yaanzisha kampeni kulinda Bwawa la Mindu

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanza kampeni ya nguvukazi kupanda miti kuzunguka Bwawa la Mindu linalotegemewa kwa zaidi ya asilimia 70 katika kutoa huduma ya maji safi na salama ili kutokausha maji hususan nyakati za kiangazi.
Kampeni hiyo ilizinduliwa mjini hapa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Amanzi.
Akizindua kampeni hiyo, Amanzi mbali na kukipongeza chuo kubuni mpango huo alisema kutokana na uharibifu wa mazingira uliopo nchini nchi inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi katika baadhi ya maeneo.
Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Gerald Monela, alisema licha ya chuo hicho kuwa na mafanikio bado kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ya baadhi ya wananchi kuvamia eneo la chuo.
Alisema licha ya chuo kushirikisha jamii kutunza mazingira, jamii imekuwa ikikiuka taratibu na kuendeleza kukata miti hovyo, uchomaji wa misitu na kufanya shughuli nyingine katika maeneo hayo.
Naye Mkuu wa Kitivo cha Misitu na Hifadhi ya Mazingira, Yonika Ngaga, alisema lengo la kuadhimisha siku ya upandaji miti ni kuipa hamasa jamii kutunza mazingira, pamoja na kulinda mipaka ya chuo isiharibiwe pamoja na mipaka ya Bwawa la Mindu.
Uzinduzi wa upandaji miti unafanyika kila Aprili mosi, lengo likiwa ni kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira.
Chanzo;Tanzania Daima 

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa