Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waathirika wa mafuriko eneo la Dumila mkoani Morogoro wameiomba
Serikali kuharakisha kuwapatia makazi ya kudumu ili waweze kuendelea na
shughuli zao kama ilivyokuwa awali.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti waathirika
hao kutoka vijiji vya Mateteni na Magole walisema bado wanaishi katika
mazingira magumu hali inayowasababisha kushindwa kufanya shughuli
mbalimbali za kiuchumi ikiwamo kilimo.
Mwenyekiti wa Kambi ya Mateteni, Mustafa Choteka
aliiomba Serikali kuwahurumia waathirika hao kwa kuharakisha kuwapatia
nyumba za kudumu kwa kuwa wanaishi katika mazingira magumu.
“Tunaishukuru Serikali na taasisi mbalimbali
ikiwamo Chama cha Msalaba Mwekundu, wametusaidia mahitaji mbalimbali,
lakini bado kuna haja ya kutuweka katika sehemu salama,”alisema Choteka.
Hata hivyo, Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu
Tanzania, Dk. George Nangale alitoa wito kwa waathirika hao kuanza
kutayarisha mashamba yao ili waweze kuwa na chakula cha kutosha huku
wakisubiri makazi ya kudumu.
“Serikali iharakishe kuwasaidia waathirika hawa
kwani bado wapo katika hali ngumu, hivyo ni vyema wakipewa maeneo ya
kudumu waliyoahidiwa mapema ili waweze kuendelea na maisha yao ya
kawaida,” alisema Dk.Nangale
Alisema Chama cha Msalaba Mwekundu kimeweza kutoa
misaada ya magodoro, vyombo, nyumba za muda (matenti) na vijana wa
kujitolea kukaa na waathirika hao kwa kipindi hiki ili kuwawapatia
ushauri nasaha.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera alisema tayari Serikali za vijiji hivyo wameshatoa viwanja kwa waathirika wa mafuriko.
“Hivi ninavyokuambia Serikali za vijiji hivi
wameshaanza kuwagawia viwanja vya kujenga nyumba zao, sisi kazi yetu ni
kuwahudumia lakini kujenga nyumba ni wao wenyewe”alisema Bendera.
Bendera alisema tangu waathirika hao wakumbwe na
adha ya mafuriko Serikali inaendelea kuwahudumia kwa kuwapa chakula na
mahitaji mengine.
“Tutaendelea kutoa mahema mapya kwa yale yanayovuja na chakula tutatoa hadi hapo wanakijiji hao watakapovuna mazao yao,”alisema.
Chanzo;mwananchi
Chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment