Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SHAMBA la Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya tatu, Fredrick Sumaye,
lililopo Kijiji cha Mvomero wilayani hapa, limetajwa kuwa chanzo cha
uhaba wa ardhi na uharibifu wa mazingira kutokana na kuwalazimisha
wananchi kukimbilia kwenye maeneo tengefu ya kutunza mazingiria
milimani.
Sambamba na madai hayo, Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imetajwa
kuchochea uharibifu wa mazingira kwa kukalia sheria ndogondogo
walizotunga wananchi kwa lengo la kupambana na waharibifu wa mazingira,
wakiwemo wavamizi.
Hayo yalibainishwa juzi kwenye mdahalo wa wananchi na viongozi
ulioitishwa na asasi ya mazingira mkoani Morogoro (Conasu) na Mtandao
wa Mazingira Tanzania (Manet) kwa hisani ya Mfuko wa Hifadhi ya
Wanyamapori Duniani (WWF) kujadili njia ya kuhifadhi pamoja msitu.
Akiongoza mdahalo huo, mwezeshaji kutoka Conasu, Ahmed Mdangu,
aliwataka washiriki kuainisha changamoto zinazosababisha milima tegemeo
kwa vyanzo vya maji na hewa safi kuharibika.
“Fursa pekee waliyonayo Watanzania ni ardhi inayowazunguka… kuna
changamoto nyingi zinazotukabili ikiwemo iliyo usoni ya Jumuia ya
Afrika Mashariki, kwa hiyo wananchi tuamke na kulinda maeneo yetu kwa
faida ya kizazi cha leo na kijacho,” alisema Mdangu.
Kutokana agizo hilo, washiriki wakiwemo Hamadi Binsaki, Paulina
Anthon na Mohamed Lundenga, walisema wamewahi kutunga sheria ndogo ya
kulinda mazingira, lakini halmashauri imezikalia na hakuna kiongozi
anayetaka kuzizungumzia.
Binsaki alisema uharibifu mkubwa umeibuka miaka ya karibuni kutokana
na eneo kubwa la kijiji hicho kupewa mwekezaji waliyemtaja kuwa Waziri
Mkuu mstaafu wa awamu ya tatu, Sumaye.
Alisema kupewa kwa eneo hilo kwa mwekezaji huyo pia kuliibua hofu
kubwa ya usalama kwa wanakijiji baada ya baadhi walioonekana kuwa
msitari wa mbele kudai uhalali huo kukamatwa na kuwekwa ndani.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment