Home » » Watumishi afya watakiwa kutoa huduma bora

Watumishi afya watakiwa kutoa huduma bora

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WATUMISHI wapya wa Sekta ya Afya nchini wametakiwa kutoa huduma bora kwenye vituo wanavyopangiwa. Pia wametakiwa kuheshimu kanuni na maadili ya utumishi wa umma na kushirikiana na wenzao katika kutoa huduma wanapokuwa kazini.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Godfrey Mtei mjini hapa jana.
Alisema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo kazi ya watumishi wa afya, chini ya Mradi wa Global Fund Round 9, unaosimamiwa na Mkapa HIV/AIDS Foundation.
Alisema Sekta ya Afya nchini inakabiliwa changamoto nyingi kama vile upungufu mkubwa wa wataalamu wa afya. Mganga Mkuu huyo alisema upungufu huo umeathiri zaidi sehemu ya vijijini, ambako wanaishi watanzania wengi.
Alitaja changamoto nyingine ni kiwango duni cha utoaji wa huduma na hilo linajidhihirisha na kuwepo kwa malalamiko mengi ya wananchi katika Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati karibu kote nchini.
Mganga Mkuu alisema changamoto nyingine ni uhaba wa rasilimali fedha za kuboresha mazingira ya kazi na pia mazingira ya watumishi kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi ya Taasisi ya Mkapa, Rahel Sheiza alisema mradi huo tayari umeajiri watumishi wa afya 460 kwa awamu mbili, wakiwemo na wakufunzi 75 katika Vyuo 14 vya Afya nchini.
Alisema watumishi 230 wa afya, waliajiriwa awamu ya kwanza kwenye Halmashauri za wilaya 35. Idadi kama hiyo waliajiriwa awamu ya pili katika halmashauri nyingine 35 nchini.
Alisema, mradi huo ulianzishwa mwaka 2010 na unatarajia kufikia tamati mwaka 2016 na umelenga kutoa wataalamu wa sekta ya afya ambao baadaye watapangiwa kwenye halmashauri nchini.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa