Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wananchi wa Kijiji cha Pwaga katika Wilaya ya Mpwapwa wamewataka
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuweka vipengele kuhusu haki za
wasichana wanaopewa mimba na kutelekezwa.
Wakichangia maoni yao katika mdahalo juu ya
utawala bora juzi, wananchi hao walisema vitu vingi vimeachwa ndani ya
Rasimu ya Katiba.
Mdahalo huo uliitishwa na Muungano wa Asasi za
Kiraia wilayani Mpwapwa, (Ngomnet) kwa ufadhili wa The Foundation for
Civil Society.
“Mambo mengine ni ya msingi kabisa. Tusipoangalia
yanaweza kutuyumbisha. Mimi nakerwa sana na tabia ya vijana wa kiume
wanaowapa mimba watoto wetu wa kike na baadaye kuwatelekeza.Hili
likiwekwa kisheria hata ndani ya Katiba litasaidia sana,” alisema Edward
Chiwanga.
Chiwanga alisema tabia hiyo imeanza kuota mizizi
katika maeneo mengi na kwamba imekuwa ikisababisha wasichana kukatisha
masomo. Alisema hali hiyo inatokea wakati wanaume hao hawachukuliwi
hatua.
Akitoa mada katika mdahalo huo, Edward Mbogo
aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kufanya uamuzi wa busara
ili kujenga nchi.
Alisema wajumbe hao wanapaswa kuhakikisha kuwa wanaondoka Dodoma wakiwa wamoja na nchi kubaki kuwa moja.
Mbogo alisema kinachosubiriwa na Watanzania si
malumbano kuhusu posho au namna ya kupiga kura ya siri au wazi, bali
katiba yenye matumaini kwa wote.
Kuhusu utawala bora, alisema bado watu wengi
hawajui jinsi ya kupata haki zao za msingi na kwamba wamekuwa wakiziomba
badala ya kuzidai.
Alisema wakati wote haki zinakwenda na wajibu hivyo kama wananchi wametimiza wajibu wao hawatakiwi kuomba haki.
Wakati huo huo, vikundi vya wanawake katika
Manispaa ya Morogoro, vimemwomba mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini,
Abdulaziz Abood kuhakikisha anatetea kupatikana kwa haki na masilahi ya
wanawake kwa namna yalivyopendekezwa na makundi ya wanawake nchini ili
yaweze kuingizwa katika Katiba Mpya.
Wanawake hao walisema hayo mjini Morogoro wakati
wakipokea msaada wa vifaa mbalimbali pamoja na hundi kutoka kwa mbunge
huyo ambayo ilikuwa ni ahadi yake kwa vikundi hivyo baada ya kufanya
ziara. Alishauri mapendekezo ya wanawake ni vizuri yakaingizwa katika
Katiba mpya kwani wao ndiyo wamekuwa na jukumu kubwa la kuelimisha jamii
na familia kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzake, Mwenyekiti wa Kikundi
cha Slab Vicoba cha Polisi, Ukende Ugula alisema suala la kuhakikisha
wanawake wanapata nafasi za viongozi nusu kwa nusu na wanaume
lizingatiwe ili kuweka usawa katika maamuzi ya ngazi zote.
Ugula alisema kuwa bado wanawake wamekuwa
wakidharauliwa na kundi kubwa la wanaume hasa wale waishio vijijini na
kukabiliwa na changamoto za kutengwa bila sababu za msingi mpaka
kusababisha vifo visivyotarajiwa katika familia.
Akikabidhi msaada huo mbunge huyo aliwataka
wanawake hao kuhakikisha wanatumia kwa manufaa ya jamii wanayoiongoza
ikiwa ni pamoja na kuinuka kiuchumi ili kuondokana na utegemezi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment