OFISI
ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa imetoa tani 105 za mahindi na vifaa
vingine kwa ajili ya watu walioathiriwa na mafuriko katika Tarafa ya
Magole, wilayani Kilosa.
Pia imetoa magodoro na mabati kwa ajili ya watu hao waliokumbwa na mafuriko Januari 22 mwaka huu.
Mkuu
wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera alitoa taarifa hiyo juzi katika kituo
cha Dakawa, Kilosa, kunakohifadhiwa vyakula na vifaa vya misaada kwa
ajili ya wananchi wa vijiji vya Kata Dumila, Msowero, Berega na Magole.
Bendera
alisema taarifa ya awali, inaonesha walioathiriwa na mafuriko kwa
wilaya ya Kilosa, Gairo na Mvomero ni watu 12,472. Kati yao hao watu
12,010 ni kutoka Tarafa ya Magole wilayani Kilosa.
“Takwimu
hizi bado ni za awali tulizomwambia Rais alipofika kuwapa pole
waathirika wa mafuriko na kutembelea eneo lote lililokumbwa na
mafuriko,” alisema.
Alisema
kwa sasa wanakamilisha kwa kuwaainisha walengwa kwa kuwaandika majina
yao, idadi ya watu kwenye kaya na wale waliobomokewa na nyumba zao na
kukosa mahala pa kuishi ili misaada iwafikie moja kwa moja.
Katika
hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart,
Scholastika Kevela amekabidhi vyakula vyenye thamani ya zaidi ya Sh
milioni 1.5 kwa waathirika wa Tarafa ya Magole.
Wakati
huo huo, Serikali imepanga kuhamisha Shule ya Msingi Magole wilayani
Kilosa, ilipo sasa katika eneo linalokumbwa na mafuriko ya mara kwa mara
kwa kujenga majengo mapya sehemu salama zaidi.
Mkuu
wa Wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo, alisema hayo juzi mbele ya Wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, iliyoongozwa na
Mwenyekiti wake, Said Mtanda ilipotemebelea Magole kwa ajili ya kutoa
pole na kusikiliza shida zao.
Wajumbe
wa Kamati hiyo walikagua majengo ya Shule ya Msingi Magole, nyumba za
walimu na jengo la Mahakama ya Mwanzo, ambayo yote yaliathiriwa na
mafuriko.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment