Upepo mkali uliovuma mithili ya kimbunga, umeezua mapaa ya
nyumba zipatazo 200 katika Mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro na
kusababisha mamia ya familia, kokosa mahali pa kuishi.
Maafa hayo yametokea wakati Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA), ikiwa imetoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua na upepo
mkali katika maeneo mbalimbali kuanzia leo hadi keshokutwa.
Katika Mkoa wa Morogoro, nyumba 183 zimeezuliwa
kutokana na upepo mkali uliojitokeza jana katika Kata za Kidatu Sanje,
Mkamba na Mkula, wilayani Kilombero.
Upepo huo uliodumu kwa takriban saa mbili, pia
umeharibu mazao na kuangusha miti ambayo mingine iliangukia kwenye
nyumba na kuzibomoa.
Taarifa kutoka katika maeneo hayo zilibainisha
kuwepo kwa majeruhi mmoja aliyeangukiwa na mti, lakini aliwahishwa
katika Hospitali ya Mtakatifu Francis, mjini Ifakara kwa matibabu.
Kwa mujibu wa habari hizo, watu waliokosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa, wamepata hifadhi kwa ndugu, jamaa na marafiki.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero,
David Ligazio, alikiri kuwa upepo uliovuma katika maeneo hayo, haujawahi
kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 iliyopita.
“Ni kweli kumetokea upepo mkali uliodumu kwa muda
wa saa mbili na baadhi ya nyumba za watu zimeathirika, watu wanaishi kwa
ndugu na jamaa zao. Kwa sasa tunaangalia namna ya kusaidia,” alisema
mwenyekiti huyo.
Katika maeneo ya Shule ya Msingi Itefa,
kulibainika kuwa vyumba vinne vya madarasa na viwili vya ofisi za walimu
vimeezuliwa kwa upepo huo ulioanza wakati tayari wanafunzi wakiwa
wameruhusiwa kurudi nyumbani.
Tofauti na ilivyotokea Kilombero, katika Wilaya ya
Same, upepo huo uliandamana na mvua kubwa yaliyosababisha mapaa ya
nyumba kuezuliwa na Barabara ya Dar es Salaam – Moshi eneo la Hedaru
kufungwa kwa muda.
Katika Kata ya Makanya, zaidi ya nyumba nane zimeezuliwa na nyingine kuanguka.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi, alisema
maafa hayo yametokana na mvua zilizoanza kunyesha tangu juzi na
kusababisha maji kutoka maeneo ya milimani kufurika katika uwanda wa
chini ambao ni tambarare.
“Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya milimani
zimesababisha maji kujaa katika maeneo ya tambarare. Nyumba zimejaa
maji, pia imeathiri ujenzi wa madaraja katika Barabara ya Same –Mombo,”
alisema.
Kujaa kwa maji katika barabara hiyo, kumesababisha
msururu mkubwa wa magari yaliyokuwa yakitoka Arusha kwenda Dar es
Salaam na Tanga.
Pia yaliyotokea Moshi Kilimanjaro na Arusha kwenda katika majiji ya ya Dar es Salaam na Tanga.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment