Home » » Nyumba 183 zaezuliwa na upepo

Nyumba 183 zaezuliwa na upepo

Zaidi ya nyumba 183 zimeezuliwa kutokana na upepo mkali katika kata za kidatu Sanje, Mkumba na Mkula wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.
Upepo huo uliodumu kwa takribani saa mbili, mbali na kuharibu nyumba 183, uliharibu pia mazao  na kuangusha miti ambayo mingine iliangukia kwenye nyumba na kuzibomoa, hivyo watu kukosa mahali pa kuishi.

Taarifa kutoka eneo la tukio zilibainisha kuwepo kwa majeruhi mmoja ambaye aliangukiwa na mti, lakini alikimbizwa hospitali kwa matibabu huku waliobomokewa nyumba zao wakihifadhiwa na ndugu, jamaa na marafiki.

Upepo huo ambao haukuambatana mvua, uliangusha miti mikubwa mingine kungoka kabisa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, David Ligazio, alitembelea maeneo yaliyokumbwa na uharibifu na kusema kuwa upepo wa aina hiyo haukuwahi kutokea katika maeneo hayo.

Katika maeneo ya  Shule ya Msingi Itefa  madarasa manne na vyumba viwili vya ofisi ya walimu pamoja na nyumba mbili viliezuliwa kwa upepo huo ambao uliibuka wakati tayari wanafunzi wameruhusiwa kurudi majumbani.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, katika Kata ya Sanje kijiji cha Msolwa Ujamaa nyumba 79 ziliathiriwa, kijiji cha Sanje nyumba 21 na mtoto mmoja alijeruhiwa kwa kushambuliwa na nyuki waliotoka katika mapango ya miti ingawa aliweza kuokolewa na wasamaria wema na hali yake inaendelea vizuri.

Katika kata ya Mkula nyumba 11 zilikumbwa na uharibifu huo na Mkamba ni nyumba 43 katika kitongoji cha Mkamba A na Mkamba  B nyumba 29.

Ligazio alisema tathmini inaendelea ili kubaini athari zaidi.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa