Mbunge wa Jimbo la Morogoro (CCM) Abdualaziz Abood
Vurugu hizo zilianza kuibuka saa 1.30 asubuhi katika Shule ya Msingi Kambarage na baadaye kuendelea katika shule nyingine za Chamwino A,B na Jitegemee, baada ya baadhi ya wazazi hao kutofautiana kuhusu kulipa au kutolipa kiasi hicho cha Sh. 50,00 kwa ajili ya kuandikishwa watoto wao masomo ya darasa la kwanza katika shule hizo. Kuibuka kwa vurugu hizo kulitokana na ziara ya kustukiza ya Mbunge Abood ya kukagua zoezi hilo la uandikishwaji wa watoto katika shule za msingi nne za kata ya Chamwino.
Akiwa katika Shule ya Msingi Kambarage, Abood alipewa malalamiko na baadhi ya wazazi kuwa watoto wao wamegoma kuandikishwa kwa madai ya kushindwa kulipa Sh. 50,000 zilizodaiwa kupitishwa na mkutano wa wazazi ulioitishwa na Diwani wa kata hiyo Joram Masenene mwishoni mwa mwaka jana.
Wakati baadhi ya wazazi wakitoa kero hiyo kwa Abood, ghafla waliibuka wazazi wengine na kudai kuwa kiwango hicho ni kweli kilipitishwa kwa pamoja katika kamati ya shule kwa ajili ya kuchangia huduma ya madawati, ulinzi na maji kwa mtoto yoyote atakayeandikishwa kuanza darasa la kwanza na kwamba wanaopinga hawakuwapo na ni wafuasi wa vyama vya upinzani.
Kufuatia hali hiyo, baadhi ya wazazi waliamua kuwarushia makonde wenzao na kudai hakuna mkutano wowote ulioitishwa kwa wazazi kupitisha mchango huo kwa kila mwanafunzi anayeingia darasa la kwanza.
Hamadi Hassan aliyenusurika kupigwa alidai kuwa walikaa pamoja na walimu wakapanga kiwango hicho cha fedha na wanaopinga ni wazazi ambao hawapendi kuhudhuria vikao vya kamati za shule mara kwa mara na kutokujua kinachoendelea katika shule wanazosoma watoto wao pamoja na changamoto zinazozikabili.
Naye Katibu wa CCM kata ya Chamwino, Dismas Makanjila, alisema wao kama chama walipinga ongezeko hilo la Sh. 50,000 ambalo lilitangazwa na diwani wa kata hiyo kwa kushirikiana na watendaji na kupendekeza kuendelea kwa kiwango cha zamani cha Sh. 30,000.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment