CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, kimesema wabunge wake
waliopo kwenye nyadhifa za uwaziri sio mizigo kwa kuwa wameonekana
kufanya kazi vizuri.
Wabunge wa Mkoa wa Morogoro ambao wamo katika nyadhifa hizo ni Mbunge
wa Ulanga Mashariki, Celina Kombani ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mbunge wa Mvomero, Amos Makalla
ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana kuhusu utekelezaji
wa ilani ya uchaguzi kwa wabunge wa mkoa huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa
wa Morogoro, Innocent Kalogerezi, alisema mawaziri hao wameonyesha
utendaji mkubwa tangu walipoteuliwa kushika nyadhifa hizo.
Alisema kutokana na hali hiyo ndiyo maana katika ziara ya Katibu Mkuu
wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana katika mikoa ya kusini hawakutajwa
mawaziri wanaotoka Morogoro katika orodha ya mawaziri mizigo.
Alisema kuwa Waziri Kombani ni mmoja wa wabunge wa mfano wa kuigwa
katika Mkoa wa Morogoro kutokana na utendaji wake katika wizara zote
alizopewa nafasi ya kuongoza na Rais Jakaya Kikwete.
Akimzungumzia Waziri Makalla, alisema kuwa naye ni mmoja wa mawaziri
wanaofanya vizuri licha ya kuwa na kipindi kifupi tangu ateuliwe
kushika nafasi hiyo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment