Home » » Athari kuwekeza katika mifumo ya kifedha isiyo rasmi

Athari kuwekeza katika mifumo ya kifedha isiyo rasmi

Katika makala ya leo kuhusiana na uwekezaji katika mifumo ya fedha isiyo rasmi nitaongelea kuwekeza katika michezo ya piramidi (PYRAMID SCHEMES). Sehemu kubwa imetokana na chanzo kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana nchini Tanzania (CMSA). Endelea…
Michezo ya kipiramidi ni mpango au mchezo wa kuchangisha fedha unaoendeshwa na mtu au kikundi fulani cha watu kwa lengo la kuwapatia wachangiaji faida kubwa ndani ya kipindi kifupi.
Michezo hii inakua kivutio kikubwa kwa wachangiaji kutokana na ahadi ya malipo ya faida kubwa ndani ya muda mfupi, bila ya wachangiaji kujihusisha kwa namna yoyote na shughuli za uendeshaji za mpango wenyewe.
Kupitia hii michezo watu mbalimbali wamepoteza fedha zao kutokana na kuwa na tamaa ya kupata faida kubwa ndani ya muda mfupi. Inawezekana kuna ambao bado wanaendelea na kuwekeza katika mifuko ya namna hii mpaka sasa, ila bado haijajulikana kwa wananchi kwa kiwango kikubwa.
Kuna wateja ambao walikuwa wanapata ushauri kutoka kwangu kuhusiana na faida zinazopatakana kutokana na uwekezaji kupitia masoko ya mitaji na dhamana, wengine walithubutu kusema bora wakapande mbegu kwani kunafaida kubwa ukilinganisha na masoko ya mitaji na dhamana na muda wa kuvuna mbegu pia ni mfupi.
Ninakumbuka ilikuwa mwaka 2008 mwishoni. Katika kupanda mbegu kuna ambao walishindwa kuvuna walichopanda, kwani watu wengi walipata hasara.
Ili kushiriki katika mpango wa piramidi, mchangiaji hutakiwa kuchangia kiasi fulani cha fedha kwa waendeshaji wa mchezo huu na anatakiwa awashawishi wengine wafanye kama yeye.
Matarajio ni kwamba kila mtu atakuwa na nafasi sawa ya kufikia kilele na kupata malipo kutokana na mchango wa wanachama wengine.
Mpango huu ni wa udanganyifu. Mpango huu hauelezi ni jinsi gani pesa zilizochangwa zinatumika vipi kuzalisha faida. Vile vile hakuna mfumo ulioandaliwa kwa kuhakikisha kwamba michango yote iliyokusanywa hutumika kwa faida ya wachangiaji.
Mpango wa aina hii unachezeshwa kwa namna ambayo fedha za kila mshiriki mpya, hutumika kumlipa mshiriki aliyetangulia.
Ili kila mshiriki aweze kulipwa, ni lazima kuwepo na washiriki wengi wapya ambao wana nia na uwezo wa kulipa fedha katika mpango. Kwa mara nyingi mchezo hufikia mwisho wake pale ambapo wachangiaji zaidi kukosekana.
Kwa mfano tuchukulie kwamba katika mchezo mmoja, mchangiaji anatakiwa kuchangia shilingi 50,000 na kupewa Shilingi 300,000 baada ya miezi mitatu. Ili kumlipa mchangiaji wa kwanza, unahitaji wachangiaji 6 katika safu ya Pili. Ili kuwalipa wachangiaji waliolipa katika safu ya pili, unahitaji wachangiaji 36 katika safu ya tatu. Katika safu ya nne, unahitaji wachangaiaji 216
Katika nchi nyingi michezo ya piramidi imewafanya watu wengi kupoteza akiba zao na baadaye kufilisika na bila ya kuwa na uhakika wanamdai nani ili awafidie hasara waliyopata. Hapa kwetu mchezo huu ni haramu. Mtu au kikundi chochote kinachochangisha mchezo huu anavunja sheria. Vivyo hivyo, mtu yeyote anayechangia kwenye mchezo huu pia huvunja sheria
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa