Home » » Viongozi zingatieni kutoa taarifa sahihi

Viongozi zingatieni kutoa taarifa sahihi

Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete aliikataa taarifa ya watu walioathirika na mafuriko yaliyotokea eneo la Dumila katika Wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro.
Wakati hayo yakitokea, naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abass Kandoro aliikataa taarifa ya fedha zilizotumika kwenye ujenzi wa mabwawa mawili wilayani Mbozi.
Taarifa iliyokataliwa na Rais Kikwete ilikuwa ikitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ambayo bila shaka iliandaliwa na jopo la viongozi wa mkoa na wilaya husika wakiwamo wakuu wa wilaya na wakurugenzi.
Katika taarifa yake Bendera alisema wananchi 12,472 walipoteza makazi, na kuongeza kwamba nyumba 1,141 zilibomoka na nyumba zingine 2,755 ziliingiliwa na mafuriko.
Bila shaka sentensi hiyo hapo juu ina utata mwingi. Ina utata kwa sababu haijawa wazi kwa kutamka ukweli wa mambo yalivyo.
Kwa msomaji yeyote wa takwimu hapo juu angependa kujua tofauti ya kati ya wakazi 12,472 kupoteza makazi na takwimu ya nyumba 1.141 kubomoka.
Baadhi ya maswali ya kujiuliza ni je wakazi 12,472 waliopoteza makazi, nyumba zao zipo? Pili je nyumba 1,141 zilizobomolewa zilikuwa za nani?
Mkuu wa mkoa anasema nyumba 2,755 ndizo zilizoingiliwa na mafuriko, sasa ziko salama ama zilibomolewa?
Hayo ni baadhi tu ya maswali ambayo kwa kweli nadhani alijiuliza sana Rais Kikwete na hatimaye kuamua kuikataa taarifa ya mkuu wa mkoa.
Kimsingi taarifa ingechanganya mambo muhimu yakiwamo ya vijiji vilivyoathirika vina watu wangapi, na walioathirika ni wangapi, nyumba zilizobomoka na idadi ya wamiliki wa nyumba na familia zao.
Hivyo nasisitiza kwamba kwa taarifa zenye utata kama hizo kutolewa mbele ya kiongozi mkuu wa nchi ni fedheha na kwa kweli wahusika lazima wajiulize sababu za kutokea mambo hayo.
Cha msingi, hata kama waandaaji wapo, lakini kiongozi atakayewasilisha taarifa mbele ya watu wengine lazima ajiridhishe kwa kuhakikisha yaliyoandikwa yana ukweli mtupu.
Tabia za kusoma hotuba ama taarifa mbele ya hadhira zilizoandikwa na watu wengine bila ya kuzipitia kwanza zina madhara makubwa.Baadhi ya madhara ni kuaibika na kudhalilika mbele ya jamii kama ilivyotokea. Hivyo msomaji lazima awe makini zaidi ya aliyeaandaa.
Hali kadhalika wapo watendaji ambao kwa makusudi wanaandaa taarifa za kupotosha kwa lengo la kutaka kuongeza idadi ya waathirika ili misaada ikitolewa wafaidi na waathirika hewa.
Utata kama huo umejitokeza mara kadhaa kwenye maeneo ya majanga na kuisababishia Serikali hasara.
Pia wapo watendaji wa Serikali ambao kwa makusudi wanaandaa taarifa za kuwasomea wakuu wa wilaya ama mikoa na hata mawaziri zikiwa na kasoro nyingi.
Wengine wanatoa taarifa za uongo hata masuala muhimu kwa jamii zikiwamo za kujua ukweli kama wananchi wanakabiliwa na njaa , kujua ukweli kuhusu magonjwa yanayosumbua wilaya ama mkoa, kujua ukweli wa kuwapo mauaji ya kutisha.
Wapo viongozi wa halmashauri ama wilaya ambao wanatoa taarifa nzuri kuhusu elimu, maji na hata afya, lakini ukichunguza ukweli ni aibu tupu.
Kwa mfano hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Kandoro naye alilazimika kuikataa taarifa iliyohusu matumizi ya fedha za kujenga mabwawa katika vijiji viwili wilayani Mbozi.
Kandoro alifika Mbozi ambako pamoja na mambo mengine alipokea taarifa za ujenzi wa bwawa la maji katika Kijiji cha Iyula na la Kijiji cha Msia.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa